Na.WAMJW-SIMIYU
Mkoa wa Simiyu utahakikisha kiasi cha shilingi Milioni 140 walizopatiwa kwa ajili ya zoezi la ugawaji kingatiba ya magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo zinatumika ipasavyo na kuwafikia watoto wote waliolengwa.
Hayo yamesemwa jana na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyonge wakati wa kikao kazi cha uhamasishaji wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kilichofanyika mkoani humo.
Mhe. Kaminyonge amesema kuwa Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote wamejipanga na kuhakikisha fedha hizo zitaleta matokeo chanya kwa watoto watakaoenda kupata kinga tiba hizo na kufikia asilimia zilizotarajiwa.
“Lengo kuu la serikali ya awamu ya sita ni kutumia rasilimali chache zilizopo katika kudhibiti magonjwa yanayowasumbua wananchi wake,hivyo kupitia mpango huu unaotekelezwa kwa pamoja kwa kuunganisha nguvu na kupunguza gharama na hivyo kuwafikia wananchi kwa urahisi”.
Hata hivyo Mhe. Kaminyonge ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wote wenye umri wa kwenda shule wapatiwe kinga tiba hizo na kuwataka waratibu wote wa afya na elimu kutoa elimu na kuwahamasisha ipasavyo wazazi kwenye maeneo yao.
Amesema dhamana ya kuwaangalia wananchi ipo juu yao hivyo wahakikishe kila halmashauri inatoa hamasa kwa jamii kwani kinga tiba hizo ni salama na zimethibitishwa na mamlaka husika hazina madhara yeyote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwela amesema wao kama watendaji wapo tayari kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Halmashauri ili kuhakikishaa zoezi hili limefanikiwa na kuwafikia watoto wote.
Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendesha zoezi hilo kwani kinga tiba hizo ni muhimu sana kwa watoto na inasaidia kuwaepusha na athari zitokanazo na magonjwa ya kichocho na Minyoo ya tumbo.
Kwa upande wa Mratibu wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Mkoa wa Simiyu Dkt. Ntugwa Nyorobi amesema mkoa wao umejipanga kikamilifu kuendesha zoezi hilo kwa hamlashauri zote za mkoa na lengo lao ni kuwafikia watoto wapatao 417,593 kwa mkoa mzima na kufikisha lengo la asilimia 85 kitaifa.
-Mwisho-
Post A Comment: