Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka leo ametembelea banda la maonesho la Chuo cha Kumbukumu ya Mwalimu Nyerere na amekipongeza Chuo hicho kwa kusema kuwa ni Chuo bora na kimefanya maonesho bora kwa kuwa na wabunifu Sita ambao wanashiriki maonesho ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya NACTE yanayoendelea mkoani Dodoma na kuwa  kupitia bunifu za wanafunzi hao  zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo leo alipozungumza na wabunifu wa Chuo hicho na kusema kuwa ofisi yake ipo tayari kuwafadhili na kutoa ili waweze kuziendeleza bunifu zao na zikishakamilika atashauriana na viongozi wenzake ziweze kutumika kwenye maeneo husika kwa kuanzia serikalini.

Mtaka amewataka wabunifu hao kuonana naye ofisini kwake baada ya kukamilika kwa maonesho haya ili aweze kuona namna bora ya kujipanga na kutekeleza ahadi ya mkoa kuwafadhili wabunifu na kufanya majaribio ya bunifu hizo katika mkoa wa Dodoma (Pilot Area).  

“Ninawapongeza sana Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa Chuo kilichoonesha bunifu bora, bunifu ambazo ni hitajio la jamii katika maisha yetu ya kila siku. Ninaahidi kuwapa ushirikiano ili bunifu hizi ziendelezwe na ziwe na tija. Wengi wenu hapa mmesema mnafanya kozi za cheti na Diploma, hivyo NACTE oneni namna bora ya kuendeleza zaidi hii kada ili Taifa liweze kufikia Malengo,”alisema Mkuu huyo wa Mkoa.


Bunifu za Chuo ambazo zinaoneshwa katika viwanja vya Jamhuri ni pamoja na mita ya maji ya malipo kabla (Pre-Paid water meter system), fimbo janja ya watu wasiiona (smart blind stick), Ubao unaojifuta wenyewe (smart Board Clean), Fimbo ya mtetemo kwa ajili ya wagonjwa wanaopoteza mawasiliano ya hali ya mwili(Parkinson), Mfumo wa uzuiaji  ajali za magari zinazotokana na kupasuka kwa matairi ya gari na mfumo wa afya ya mgonjwa wa kiarusi. (Paralised patient system).


Imeandaliwa na:

KITENGO CHA HABARI NA MAHUSIANO

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

30.05.2021

Share To:

msumbanews

Post A Comment: