Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amekabidhi kiasi cha shilingi Milioni 11 kwa vituo vya kulelea watoto yatima na kwa Bw.  Allan Shomari,  mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu  aliyewahi kuchezea timu za General Tyre  na Yanga.


Makabidhiano ya vituo vya watoto yatima yamefanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa ambapo Kituo cha watoto yatima kinachosimamiwa na Msikiti wa Masjid Senta kimepatiwa shilingi Milioni 5 na kituo cha watoto walemavu kilicho chini ya Kanisa Katoliki Monduli(St.John Paul Rehabilitation Center) kimepatiwa shilingi Milioni 5.


Mhe. Mkuu wa Mkoa  alifika pia nyumbani kwa mchezaji wa zamani  wa Yanga, Bw. Allan Shomari na kumkabidhi shilingi Milioni 1. Mhe. Kimanta aliahidi  pia kutoa mchango  binafsi wa shilingi laki 5 kwa Bw. Allan Shomari.


Mhe. Kimanta amesema fedha hizo alizokabidhi zimetolewa na Shirikisho la  Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapato yaliyopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Hisani  kati ya timu za Simba na Namungo iliyochezwa Jijini Arusha katika  uwanja wa Sheikh Amri Abeid tarehe 30 Agosti, 2020.


 Mhe. Kimanta ameviasa vituo hivyo vya watoto kuhakikisha  fedha hizo zinatumika kwa maendeleo ya vituo vyao na si vinginevyo.


Mhe. Kimanta ameishukuru TFF kwa mchango huo wa kuwasaidia watoto wa vituo hivyo na kwa msaada walitoa kwa aliyekuwa mchezaji  wa zamani wa Timu ya Yanga, Bw. Allan Shomari.


Mhe. Kimanta ametoa  rai kwa wadau wengine kujitokeza kuvisaidia vituo vya watoto yatima na wenye ulemavu na pia kujitokeza  kumsaidia  Bw. Allan  Shomari ambaye ni mlemavu wa macho.


Akizungumza kwa niaba ya  TFF,  Mwenyekiti wa TFF Mkoa wa Arusha Bw.  Zakayo Mjema amesema  fedha hizo zimetolewa kwa vituo vya watoto yatima kama  mchango  wa TFF kwa jamii na ni imani yake kuwa vituo hivyo vinaweza kuzalisha wachezaji wazuri wa baadae kwa manufaa ya Taifa letu. 


Bw. Mjema ameongeza pia kuwa michezo ina fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa vijana na wao kama TFF Mkoa wa Arusha wataendelea kutoa misaada kwa watoto hao ikiwemo kuwapatia mipira ya kuchezea.


Ametoa wito kwa wadau wengine kuwasaidia wachezaji wa zamani kama walichofanya kwa Bw. Allan Shomari kwa vile bado wapo wengi mitaani wanaohitaji  msaada kama huo.


Akitoa neno la shukrani, Bw. Allan Shomari  ameushukuru uongozi wa TFF  na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Kimanta kwa msaada huo waliomkabidhi ambao utamsaidia hasa kwenye matibabu yake ya Macho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: