Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naghenjwa Kaboyoka akiwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa matumizi mazuri ya fedha za Serikali katika kutekeleza miradi ya usambaji umeme wilayani Manyoni mkoani Singida baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo leo. Kushoto ni Makamu .wa kamati hiyo, Japhet Hasunga na kulia ni Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na REA wakiwa kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlelwa, Elias Deogratius, akizungumzia mafanikio wanayopata baada ya kuwekewa umeme wa REA.
Mkazi wa Majengo John Joshua akiishukuru Serikali na REA kwa kuwapelekea umeme.
Juma Amran akiipongeza REA kwa kupeleka umeme katika Shule ya Sekondari ya Mlelwa.
Fundi Sanifu wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Wilaya ya Itigi, Godfrey Byamungu, (kushoto) akitoa taarifa kwa kamati hiyo kuhusu mradi wa maji wa Kisima kilichopo eneo la Raundi Abauti mjini humo.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naghenjwa Kaboyoka amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa matumizi mazuri ya fedha za Serikali katika kutekeleza miradi ya usambaji umeme wilayani Manyoni mkoani Singida.
Kaboyoka ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti leo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikitembelea miradi ambayo imetekelezwa na REA katika wilaya hiyo.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni uwekaji wa umeme katika Kiwanda cha Qstek ambacho kitakuwa kikichakata mafuta ya alizeti, Shule ya Sekondari ya Mlelwa na Kisima cha maji kilichopo eneo la Raundi Abauti Itigi mkoani humo.
" Tumekuja kutembelea miradi hii ili tujiridhishe kwa macho na kuona uhalisia wa fedha zinazotolewa na Serikali kama zinatumika ipasavyo tunawapongeza REA kwa kazi nzuri mliyoifanya." alisema Kaboyoka.
Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo alisema wizara hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijiji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Singida.
" Mradi unaotekelezwa kwa sasa mkoani Singida ni mradi wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza." alisema Kalemani.
Dkt. Kalemani alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kitongoji hapa nchini kinapata umeme ambapo ametoa wito kwa wananchi kuingiza umeme katika nyumba zao kwa bei ya Sh.27,000 tu hata kama wanaziona mbaya ili mradi wawe wanaishi humo.
"Niwaombe watanzania kila penye mradi wa wananchi unaohitaji umeme waweke nishati hiyo kwani itawapunguzia gharama ya kuiendesha na kuwa suala la wananchi kupata umeme ni la lazima." alisema Kalemani.
Mkazi wa Majengo wilayani humo, John Joshua aliishukuru Serikali na REA kwa kuwapelekea umeme lakini akaomba changamoto ya kukosekana kwa nguzo iangaliwe.
Juma Amran aliipongeza REA kwa kupeleka umeme katika Shule ya Sekondari ya Mlelwa na akaomba wasaidiwe kupata maji kwani hiyo ndiyo changamoto yao kubwa.
Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari ya Mlelwa, Elias Deogratius alisema baada ya kuwekewa umeme ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kupata muda wa kutosha wa kujisomea vizuri.
Post A Comment: