Mwandishi Wetu, Arumeru
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis ameyaagiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kuhakikisha miradi yanayoisimamia inalenga kuwasaidia wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha alipotembelea mradi wa Shamba Darasa unaoendeshwa na Shirika Best Agriculture Pratice (BAP) aliokwenda kuona namna Shirika hilo kinavyotoa elimu ya Kilimo cha kisasa kwa Wananchi.
"NGOs ni lazima kushirikiana na kuwawezesha wananchi kujiletea Maendeleo yao. Sio mbaki hapa tu, mkawatembelee huko vijijini wafundishwe mbinu za Kilimo za kisasa wakishapata mazao bora watapata chakula cha kutosha na kuuza" alisema.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na NGOs kuhakikisha wananchi wanafaidika na miradi inayotekelezwa na Mashirika hayo ili iweze kuleta tija kwa wananchi hao.
“Nisema sisi tutaendelea kushirikana na NGOs kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Mashirika haya inasaidia wananchi” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuendelea kufuata Sheria, Kanauni na Taratibu wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo wanayofanyia kazi.
Amesema NGOs zina mchango mkubwa sana katika jamii hasa kuwawezesha makundi maalum kujikwamua kiuchumi haswa wanawake ambao wana jukumu kubwa la kulea familia na jamii kwa ujumla.
Amewaasa wanawake kuwa mabalozi kwa wenzao na kuwasaidia kupata elimu mbalimbali ikwemo juu ya kilimo bora na cha kisasa kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga amezitaka NGOs nchini ziendelee kufanya kazi kwa tija zaidi ili ziweze kusaidia wananchi kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkuu wa Shirika la Best Agriculture Pratice Nicodemas Mabula amesema kuwa Shirika lake litatekeleza agizo la Naibu Waziri kwa kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora kwa wananchi ili waweze kulima kwa tija na kujikwamua kiuchumi.
Naye mmoja wa mnufaika wa elimu inayotolewa na Shrika hilo Bi. Eli Tiayo ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha inasimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kusaidia wananchi hasa wanawake.
Amesema elimu wanatoipata imewapa mwanga wa kufanikisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na kuzika familia na kusomesha watoto.
" Sisi tumeweza kusomesha watoto hadi vyuo Vikuu kutokana na kazi hizi na sasa wamefanikiwa wameajiriwa na kujiajiri wanaendelea kutulea sisi"
Ziara ya Naibu Waziri inalenga kutembelea na kukagua shughuli zinazosomamiwa na Wizara ya Afya ( Idra Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Sekta inayosimamiwa na Naibu Waziri huyo.
MWISHO
Post A Comment: