Na.Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali inaendelea na utekeleza wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JNHPP-Julius Nyerere Hydropower project) kwa gharama ya TZS Trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kwa gharama ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine ambayo itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya biashara na uwekezaji.
Mnamo Desemba 8, 2019, Rais wa Awamu ya Tano Hayati, Dkt. John Magufuli alizindua ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo, ukarabati wa meli na ujenzi wa chelezo katika lango la biashara na kiuchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 153.
Meli ya “MV Mwanza Hapa Kazi” itakayogharimu shilingi bilioni 89, ni mradi wa ujenzi ambao unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya GAS ENTEC wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kutoka Tanzania. Meli hii itakuwa mbadala wa meli ya MV Bukoba ambayo miaka 25 iliyopita ilizama na kupoteza maisha ya Watanzania wengi. Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 Rais wa Awamu ya Tano, Hayati, Dkt John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya ziwa kuwa atajenga meli kubwa kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo lakini pia kuimarisha usafirishaji upande huo wa Tanzania kwani kuna fursa nyingi za biashara, anaeleza Meneja Mradi Mhandisi, Vitus Mapunda.
Katika moja ya Hotuba zake akiwa ziarani Jijini Mwanza 2019, Hayati Magufuli alisema “Ni miaka 23, Baada ya kuzama meli ya MV Bukoba mwaka 1996, miaka mingi imepita, lakini pia kuharibika kwa meli ya mizigo kumekuwa na tatizo kubwa katika sekta ya usafarishaji kwa wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli za uchumi na uzalishaji kanda ya ziwa”.
Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Jemedari, Samia Suluhu Hassan, inaendelea na utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao uliambatana na miradi mingine kama vile ukarabati wa meli ya Mv Victoria uliogharimu shilingi bilioni 22.7, Mv Butiama bilioni 4.9, ambapo ujenzi wake ulitekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya KTMI kutoka Korea Kusini huku ujenzi wa chelezo uliogharimu shilingi Bilioni 36.4, ukitekelezwa na Stx Engine ikishirikina na SAE Kyong kutoka Korea Kusini. Kati ya miradi hiyo, ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli mbili umekamilika na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ukiwa umefikia asilimia zaidi ya 50, na miradi yote hii itagharimu shilingi bilioni 153.7, baada ya kukamilika na miradi yote hii inatekelezwa kwa pesa za Watanzania.
MV Mwanza Hapa Kazi tu, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400, magari makubwa 3 na magari madogo 20, huku ikiwa na urefu wa mita 92, ambapo MV. Victoria ikibeba abiria 1,200, mizigo tani 200 na MV. Butiama ikibeba abiria 200 na mizigo tani 100. Meli zote tatu zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 2,600 na tani 700 za mizigo, kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo katika ukanda huo.
“Ni wazi kuwa utekelezaji wa miradi hii utakaogharimu shilingi bilioni 153 utasaidia sana kutatua tatizo la usafirishaji kwa wananchi wanaoishi ziwa Victoria, siyo tu hapa nchini bali hata kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa hiyo ni miradi ambayo ina manufaa kwa uchumi wetu”, Hayati, Dkt. John Magufuli.
Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita inaeleza kuwa ujenzi wa mradi huo mkubwa MV Mwanza Hapa Kazi Tu, utafungua ukanda huo kibiashara na kusaidia kukuza pato la taifa, kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano Serikali ya sasa imejitabanaisha kuendelea kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti lukuki.
Sekta hii ya usafirishaji kwa njia ya maji imekuwa muhimu sana na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Shirika la Huduma za Meli Tanzania (MSCL) wamekuwa na usimamizi madhubuti ili kukuza sekta hiyo kwani ni nyenzo kubwa katika uchumi.
Kampuni ya Huduma za meli iliyoanzishwa na Hayati Baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere kwa sasa inafanya kazi kubwa baada ya Hayati, Dkt. Magufuli kuingia madarakani na kuiongezea nguvu kifedha na kiutendaji. Kijiti hicho kwa sasa kipo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwani hapo mwanzo ilikuwa na meli 14 ikiwemo meli ya utalii lakini ilikuja kuanguka kutokana uongozi mbovu, vitendo vya wizi na ubadhilifu wa mali za umma na kufanya meli zote 14 kufa na kubaki na moja tu.
TPA imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa Bandari mbalimbali nchini zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza pamoja na bandari zake ndogondogo za Kemondo, Bukoba, Kwemukwikwi na Nyamirembe kwa upande wa kanda ya ziwa, na Bandari ya Kigoma.
Mhandisi Mapunda anaeleza kuwa Ujenzi wa Meli mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu” umefikia asilimia 53 tofauti na sasa ujenzi unaendelea vyema ili kuwawezesha wafanyabiashara wa ukanda huo kuwa na nafuu ya usafiri na usafirishaji mizigo baada ya mradi huo kukamilika.
Utekelezaji wa miradi hiyo umeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na bado zinaongezeka kwa kadri siku zinavyosonga mbele katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa kwa kanda ya ziwa.
Ujenzi wa Meli hii Kubwa ni utekelezaji wa ahadi na kufanya maono ya Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa kwa ukanda huo wa kiuchumi wa Tanzania, na alijenga MV Bukoba iliyokuja kuzama mwaka 1996 na kuleta ugumu wa sekta ya usafirishaji kutumia Ziwa Victoria na sasa Serikali inayaishi maono ya Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, baada ya kujenga MV Mwanza Hapa Kazi Tu.
Post A Comment: