Afisa Maliasili katika halmashauri ya Itigi, John Makotta akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Madiwani wa Baraza hilo kuhusiana na tembo waharibifu pamoja na simba.
Madiwani wa Halmashauri ya Itigi mkoani Singida wakiwa kwenye kikao cha Baraza hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Mhe. Hussein Simba akifungua KIkao cha Baraza la Madiwani hivi karibuni
Na Abby Nkungu, Itigi
WAKULIMA katika halmashauri ya Itigi Mkoani Singida wameshauriwa kupanda pilipili na kutundika mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba yao kama njia mojawapo ya kudhibiti tembo wanaoshambulia mazao ya chakula na kuleta uharibifu mkubwa hali inayoweza kusababisha janga la njaa.
Mwito huo ulitolewa na Ofisa Ardhi na Maliasili katika halmashauri hiyo, John Makotta wakati akijibu hoja za madiwani kwenye kikao cha Baraza, waliolalamika kuwa mashamba mengi ya wakulima katika kata zao huvamiwa na tembo kiasi cha kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.
Katika hoja yake Diwani wa kata ya Kitaraka, John Subeti alisema licha ya kutoa taarifa kwa idara husika kila mara tembo wanapoingia kwenye mashamba, hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kuwadhibiti na kwamba bado wanaendelea kuharibu mazao ya chakula na biashara hali inayoweza kuleta athari kubwa kiuchumi.
Naye Diwani wa kata ya Ipande, Kedimon Mpondo alisema kuwa yapo madhara makubwa yanayojitokeza kwenye kata zilipo jirani na maeneo ya hifadhi kutokana na uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo na mifugo kuliwa na simba.
Madiwani hao waliungwa mkono na wenzao kutoka kata mbalimbali wakiomba Mamlaka husika kwenda haraka maeneo yenye wanyama hao kuwaondoa ili kuwanusuru wananchi kukumbwa na janga la njaa.
Akijibu hoja hizo, Makotta alikiri kuwa upo mfumko wa wanyapori wengi wanaovamia mashamba ya watu na amekuwa akijitahidi kuomba msaada wa askari mara kwa mara kutoka kwenye Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati (KDU) kwa ajili ya kwenda kuwafukuza.
"Idara yangu inakabiliwa na changamoto ya upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kwa hivi sasa nipo peke yangu pia, kuna uhaba wa vitendea kazi. Lakini, kwa kusaidiana na maaskari wa KDU huwa najitahidi kufika kwenye kila tukio mara ninapojulishwa" alisema Makotta na kuongeza;
Simba ni rahisi kuwahamisha kwa gari na kuwapeleka maeneo mengine lakini si rahisi kuhamisha tembo. Ili kuwadhibiti tembo kufika kwenye mashamba yenu, nashauri wakulima walime pilipili kando kando ya mashamba au kutundika mizinga ya nyuki. Mbinu hii inasaidia sana kuwazuia tembo kufikia mashamba".
Alisema njia nyingine ya kudhibiti wanyama wote waharibifu ni kuwaua kwa risasi au kwa njia nyingine yoyote lakini akatahadharisha kuwa ni lazima taarifa itolewe kwenye idara ya Maliasili kila anapouawa tembo au simba.
"Hakikisheni kila anapouawa mnyama nyara zote za Serikali kama meno na mkia kwa upande wa tembo na ngozi na kucha kwa upande wa Simba zinaondolewa na kukabidhiwa idara ya Maliasili" alisema na kusisitiza kuwa wananchi wasigawane nyama ya mnyama anayeuawa bila ruhusa kutoka Maliasili.
Post A Comment: