MBUNGE wa Jimbo la Kisesa Mh Luhaga Mpina akichangia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia bungeni Jijini Dodoma


Mtakumbuka kuwa wakati nachangia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai alisema muda wa dakika 10 haukunitosha kutoa mchango wangu na hivyo kuelekeza labda ingepatikana zaidi ya nusu saa ili niweze kutoa mawazo yangu kuhusu mfumo wa elimu yetu nchini.

Hivyo kwa heshima na unyenyekevu mkubwa napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mhe. Spika kwa kutambua uzito wa hoja yangu na ndio maana nimeona nikutane na wanahabari ili muweze kufikisha mawazo hayo kwa umma kama alivyoelekeza Mhe. Spika Job Ndugai.

Pamoja na kazi kubwa iliyofanyika na Serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli ya kuongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020 na shule za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi 5,330 mwaka 2020 na kuongeza idadi ya madawati kutoka 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207.

Licha ya mafanikio hayo makubwa bado kuna upungufu wa miundombinu ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, maabara, vyoo na madawati. Vile vile mahitaji ya ujenzi wa shule mpya ni mkubwa kwa kuwa bado wanafunzi wengi wanasafiri kilomita nyingi kufuata shule.

Mfano katika Jimbo langu la  Kisesa Kata na  vijiji vya Mwabusungu, Mwamashimba, Mwababili, Mwasungura, Mwakisandu, Mwashata na Sakasaka wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita 10 mpaka 20 kwa siku kufuata masomo hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi, tatizo hili linakuwa kubwa zaidi kipindi cha masika ambapo mvua na mito hujaa na kuwazuia kufika shuleni hali inayopelekea kushuka kitaaluma na wengine kuamua kuacha masomo na hivyo kukosa haki yao ya kupata elimu.

Nashauri Serikali ianishe mahitaji na kutenga fedha za kutosha kumaliza tatizo hili sugu ambalo limekuwa kikwazo na  mwiba mkali kwa utoaji elimu nchini.

Tunalo tatizo kubwa la muda mrefu la magofu ya madarasa, nyumba za walimu, vyoo, maabara na mabweni ambapo wananchi walishakamilisha kazi yao na kusubiri mchango wa Serikali, Waziri atuambie ni lini magofu haya yatakamilishwa ili kuunga mkono nguvu za wananchi na kuwezesha miundombinu hiyo kutoa huduma na kuondoa upungufu uliopo.

Mfano katika Jimbo la Kisesa jumla ya maabara 10 ambazo zimejengwa hadi hatua ya kupauliwa, ujenzi na uwekaji wa vifaa haujakamilika kwa zaidi ya miaka 8 sasa na hivyo kuwakosesha wanafunzi wetu kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi.

Shule nyingi za msingi na sekondari zinakumbwa na tatizo kubwa la upungufu na vyoo vya kisasa ambao unapelekea usumbufu mkubwa kwa wanafunzi kukosa huduma hiyo muhimu, tatizo hili limekuwa kubwa zaidi kutokana na vyoo vilivyopo kujaa mara kwa mara na kupelekea kuanzisha ujenzi mpya kila baada ya miezi 6 hadi mwaka 1.

Sio tu vyoo vilivyopo vinaisababishia gharama kubwa Serikali ya ujenzi wa mara kwa mara bali shule zetu zimekuwa chanzo cha magonjwa kwa watoto na kuwapa usumbufu mkubwa wa kuchukia masomo na kuanguka kitaaluma.

Kwanini Serikali isitenge fedha za kutosha kujenga vyoo vya kisasa katika shule zote za msingi na sekondari na kujenga madampo pamoja na kununua  magari ya  maji taka ili kumaliza tatizo hili sugu ambalo litaondoa usumbufu, magonjwa na kupandisha ufaulu wa wanafunzi.

Utafiti, suala la utafiti halijapewa kipaumbele cha kutosha na Serikali  taasisi zetu za utafiti hazijawezeshwa vya kutosha kutekeleza majukumu yake na hivyo kupelekea mambo muhimu ya kitaifa kukosa taarifa za utafiti na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo nchini.

Kuna shida kubwa ya uandaaji wa ajenda za utafiti nani anayeandaa, vigezo gani vinavyotumika na shirikishi kwa kiasi gani na zinawahusu akina nani kutimiza wajibu huo?

Kwa kuwa Taasisi za Serikali, binafsi na wadau wengine wamekuwa wakifanya tafiti katika maeneo mbalimbali na baada ya tafiti hizo kukamilika hufungiwa kwenye makabati badala ya kuwafikishia watuamiaji. Ni lini makabati hayo yaliyobeba tafiti hizo yatafunguliwa? kwanini Serikali isianzishe kanzidata (database) za utafiti kwa kila sekta na kuziorodhesha tafiti hizo ili kurahisisha utunzaji, usambazaji na utumiaji wa tafiti  hizo.

Hivi sasa wigo wa utafiti ni mdogo sana kwa kuwa ni tatifi chache  zinazofanywa na kujulikana serikalini na kwa wadau kwa mfano nilipokuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  tulifanikiwa kuanzisha Ajenda za Taifa ya Utafiti wa Mifugo na Uvuvi, upande wa mifugo tulianzisha (National Livestock Research Agenda 2020-2025). Uwepo wa ajenda hiyo umesaidia katika kutoa mwongozo kwa Taasisi za umma na binafsi, vyuo na watafiti wengine kuzingatia vipaumbele vya Taifa katika tafiti za mifugo.

Pia tulianzisha Kanzidata ya Tafiti za Mifugo (Database of Livestock Research) ambao umesaidia kuweza kukusanya taarifa za tafiti za mifugo kutoka tafiti 11 mwaka 2015 hadi tafiti 433 mwaka 2020. Aidha, Kanzidata hiyo imeruhusu matumizi ya matokeo ya tafiti za wanafunzi wa Shahada za Uzamili ( Masters ) na Uzamivu (PHD) katika uendelezaji wa Sekta ya mifugo.

Ili kuweka usimamizi thabiti tulitunga Kanuni za kusimamia tafiti katika Tasnia ya Mifugo (Livestock Research Regulations, 2020) ambazo zimesaidia katika kutoa miongozo ya namna ya kufanya tafiti, usambazaji wa taarifa za tafiti na matumizi ya tafiti hizo. Kanuni hizo hazikuwahi kuwepo katika miaka ya nyuma ambapo kulipelekea kuzorota kwa shughuli za utafiti nchini.

Zoezi hili ni muhimu kufanyika katika taasisi zote za utafiti ili kuleta ufanisi zaidi.

Kwanini tafiti za zinazofanywa na vijana wa shahada ya uzamili (Master’s) na Uzamivu (PHD’s) zitumike tu kukamilisha masomo na kufaulu na sio tafiti hizo kusaidia kutoa majawabu ya matatizo yaliyopo nchini ya kiuchumi na kijamii. Hivi inawezekana kweli utafiti wa ngazi ya Master’s na PHD’s ukaishia kutupwa kwenye makabati?

Kwanini Serikali isiweke utaratibu mzuri wa kuzitambua na kuziorodhesha tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa Master’s na  PHD’s na kuzifikisha kwa watumiaji kwa manufaa ya taifa.

Tunazo taasisi za utafiti za Mifugo (TALIRI), Uvuvi (TAFIRI), Kilimo (TARI), Misitu (TAFORI), Wanyamapori (TAWIRI), Afya (NIMR), NBS na Costech lakini muunganiko wa kiutendaji ni mdogo ni muhimu kutazama sheria zake upya ili kuweka misingi ya kisheria kwa kutoa miongozo, wajibu na majukumu kwa watafiti wote kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na ajenda ya utafiti ya kitaifa. Tunajua baadhi ya taasisi zimejielekeza zaidi katika tafiti za nje ambazo zingine hazina faida yoyote katika taifa.

Hali ya upatikanaji wa Ajira na Ujuzi nchini

(i) Hakuna tafiti zilizofanyika zinazoanisha mahitaji ya soko la ajira ambazo zingewezesha vijana wetu kuchagua michepuo ya masomo inayoendana na mahitaji ya ajira, vijana hawajui wachague michepuo gani kulingana na mahitaji ya soko la ajira, nini kilichowashinda Wizara ya Elimu kufanya utafiti katika eneo hili ili kuweka wazi maeneo yenye ajira kubwa na ambayo hayana ajira ili vijana wazingatie katika uchaguzi wao.

Kijana anaomba kusoma uhasibu, biashara, uchumi, ununuzi bila kujua wenzake waliosomea masomo hayo na kupata digrii wana zaidi ya miaka kumi bila kupata ajira laiti wangekuwa na taarifa hizo wangefanya chaguo sahihi katika masomo yao.

(ii) Mkakati wa kuandaa vijana wenye ujuzi maalum bado wa kusuasua na kasi yake ni ndogo kukidhi mahitaji ya soko mfano ni vijana tu pekee wanaosomea udaktari wa binadamu ndio wanaopewa fursa ya kufanya  ‘interns’ huku wanataaluma wengine wa mifugo, uvuvi, kilimo, misitu, biashara, uhasibu, uchumi, uhandisi, ununuzi wakibaguliwa katika zoezi hilo.

(iii) Mafunzo kwa wakufunzi na wahadhiri wa vyuo hayawezeshi kutoa wahitimu wenye ujuzi mkubwa katika taaluma husika,  mfano hivi sasa wakufunzi wanaobakizwa vyuoni kufundisha ni wale waliopata ufaulu wa juu kwa kuwa na A’s nyingi, wakufunzi hao wanakuwa hawajapata mafunzo kwa vitendo.

Unakuta mkufunzi na wahadhiri wa somo la biashara hajawahi kufanya biashara yoyote wala kusimamia kampuni lolote la biashara anawezaje kutoa taaluma bora. Kwanini tusiweke utaratibu mzuri zaidi wa kuandaa kikamilifu wakufunzi wetu ili kuwawezesha kutoa elimu bora zaidi kwa vijana wetu.

(iv) Hakuna ufuatiliaji wa vijana wanaohitimu mafunzo katika vyuo hapa nchini (tracer study) nani anayefuatilia vijana hawa baada ya kuhitimu mafunzo wanaenda wapi, je wameajiriwa, je wamejiajiri au wako kwa shangazi mjini wakihaha kutafuta ajira kila uchao. Wizara ya Elimu kila leo inajivunia kuongezeka kwa udahili lakini maswali magumu ya vijana hawa wanakoenda baada ya kuhitimu hayaulizwi na kujibiwa.

Mfano nilipokuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  tulielekeza Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA)  kufanya utafiti wa ajira za wahitimu wa vyuo vya mifugo nchini kutoka mwaka  2014 hadi mwaka 2019 katika kipindi tajwa wanafunzi 8,132 walihitimu masomo katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada ambapo matokeo wahitimu 776 tu sawa na asilimia 9.5 ya wahitimu wote ndio waliofanikiwa kuajiriwa na kujiajiri, Asilimia 90.5 ya Wanafunzi hawajulikani kazi wanazozifanya baada ya kuhitimu masomo yao.

Kama Wizara ya Elimu ingekuwa inafanya tafiti hizi kwa kila sekta ingeweza kuandaa miongozo, sera na sheria nzuri za kusimamia elimu nchini, kutelekeza jambo hili linatupotezea uelekeo na kutengeneza mzigo mkubwa  wa vijana wasiokuwa na ajira nchini.

(v) Masomo yanayotoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi hayafundishwi mashuleni na vyuoni, nini kilichosababisha somo la kilimo kufutwa mashuleni? Unaandaa vijana darasa la saba na sekondari ambapo zaidi ya asilimia 70 hurudi na kutegemea kilimo, mifugo na uvuvi  chakushangaza shughuli wanayokwenda kufanya hawafundishwi. Kwanini somo la ujasiriamali halifundishwi mashuleni na vyuoni kwa kila kozi ili kuwapa maarifa ya kujiajiri na kujitegemea wahitimu wa kozi zote hasa katika kipindi hiki cha uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

(vi) Hitaji la kuboresha mitaala kulingana na soko la ajira imekuwa changamoto ya muda mrefu ambapo ufumbuzi wake umekuwa wa kusuasua, haileweki ni kwanini tatizo hili halipewi kipaumbele licha ya maombi ya muda mrefu ya wadau, viwango vya ujuzi vya watafuta ajira viko chini ya viwango vinavyohitajika na waajiri, nguvu kazi kubwa ya nchi ina kiwango kidogo cha ujuzi ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika kufikia maendeleo  endelevu ya viwanda.

 (vii) Mikakati na mipango ya Serikali inakinzana na sera ya vijana kujiajiri mfano uanzishawaji wa Vyama vya Ushirika ( AMCOS ) katika ununuzi wa mazao ya pamba, choroko na ufuta ambapo wananchi wanalazimishwa kuuza mazao yao katika AMCOS pekee na si vinginevyo, kabla ya hapo mazao yaliuzwa moja kwa moja katika soko huria lililojumuisha mtandao mkubwa wa vijana, hivyo utaratibu wa AMCOS wa sasa umeua ajira nyingi za vijana nchini.

Mfano mwingine ni Serikali na taasisi zake kuwa na madeni ya muda mrefu ya wakandarasi na wazabuni, jambo hili limekuwa mwiba na machinjio ya ajira za vijana wanaojishughulisha na biashara wanapotoa huduma serikalini hawalipwi fedha zao kwa wakati hali inayopelekea kufilisika, kufunga biashara na kuua ajira. Inashangaza Serikali iliyopania vijana wake kupata ajira inajigeuza  kuwa mhujumu wa ajira hizo. Jambo ambalo ni kinyume na  Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5.

Nakiri kwamba ni tafiti chache sana zilizokwisha fanyika katika eneo la ajira na ujuzi na hata hizo chache utekelezaji wa mapendekezo yake umekuwa  si wa kuridhisha. Mfano Utafiti wa Tume ya Mipango wa mwaka 2014 kuhusu maendeleo ya ujuzi utakaoiwezesha Tanzania kuwa na uchumi imara na shindani ifikapo mwaka 2025, utafiti huo ulibainisha kuwa kuna tofauti kati ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na ujuzi unaotolewa na taasisi za elimu na mafunzo, utafiti huu unabainisha kuwa viwango vya ujuzi viko chini ya viwango vinavyohitajika na waajiri na watafuta ajira wengi wana upungufu katika stadi za kazi.

Licha ya changamoto zote nilizozieleza bado Walimu, Wakufunzi, na Wahadhiri wetu wanafanya kazi nzuri ya kutoa taaluma nchini na nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana.

Nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi kuendeleza mapambano ya kuitafuta elimu kwani elimu ni ufunguo wa maisha na tusikubali kukatishwa tamaa, Maandiko matakatifu yanasema (Biblia takatifu) Kitabu cha Methali 4:13 inasema “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake, Mshike, maana yeye ni uzima wako”.

Pia Aya ya kwanza ya Quran Tukufu imesisitiza kuhusu elimu na masomo na umuhimu wa kalamu. Umuhimu huu ni mkubwa kiasi kwamba uislamu unasema ni faradhi au lazima kwa muislamu mwanaume na mwanamke kutafuta elimu. Riwaya za Kiislamu pia zinamuusia mwana adamu kutafuta elimu na masomo hadi kwenye maeneo ya mbali zaidi duniani.

Mbali na hayo uislamu unasema utafutaji wa elimu unapaswa kuendelea katika kipindi chote cha maisha ya mwanadamu . Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW  anasema Tafuteni elimu kutoka Susu hadi Kaburini moja ya sababu ambazo zimepelekea uislamu kuzingatia sana suala la elimu ni hii kuwa elimu hufungua milango ya ujuzi na kumuwezesha mwanadamu kupata maarifa zaidi kumuhusu Mwenyezi Mungu.

Kama vitabu vitakatifu vilivyotuambia kuhusu umuhimu wa elimu sisi ni kina nani hadi tuanzishe mjadala na kubeza umuhimu wa elimu katika maisha ya mwanadamu na nchi,  Wote mtakumbuka katika siku za hivi punde ndani na nje ya Bunge kumeibuka mjadala unaotafsiriwa kulenga kubeza umuhimu wa elimu na kwamba watu waliofanikiwa hawakwenda shule. Mjadala huu hauna afya kwa mustakabali wa taifa letu kwa kuwa umuhimu wa elimu hauna mbadala.

Kama viongozi tunapaswa kutumia muda mwingi kuangalia changamoto za mfumo wa elimu unaotolewa nchini na kuzitatua badala ya kubeza umuhimu wa elimu.

Hawa watu wanaobeza umuhimu wa elimu na uwezo wa watanzania katika kupigania maendeleo yao waulizwe ni utafiti gani uliofanywa unaosema kuwa wasomi wa nchi hii hawana mchango mkubwa katika taifa.

Ni nani asiyejua michango mikubwa inayotolewa na wataalamu wetu katika sekta na nyanja mbalimbali za Ujenzi, Afya, TEHAMA, Kilimo, Elimu, Maji, Mifugo, Uvuvi, usafirishaji, ufundi  na Misitu na nk, hivi ni nani anayefanyiwa upasuaji wa moyo hospitali na mtu asiyesoma, mageuzi makubwa ya TEHAMA ambayo yamerahisisha mawasiliano na ukusanyaji wa mapato ya Serikali nayo yamebuniwa na watu wa wasiosoma?, Madaraja makubwa tunayojivunia yaliyopo nchini mfano Kigongo Busisi, Flyover Ubungo, Daraja la Kigamboni na Magorofa makubwa yanayojengwa nchini yamebuniwa na kujengwa na watu wasiosoma?

Ndege na Meli zetu zinarushwa na kuendeshwa na watu wasiosoma?, Hata wanaojivunia kuwa ni matajiri bila elimu waulizwe hizo  biashara na shughuli zao zinaendeshwa na wasiosoma? Waulizwe hiyo mipango ya biashara, mauzo, utunzaji wa fedha zinafanywa na watu wasiosoma?.

Mijadala ya namna hii ikiruhusiwa iendelee katika taifa letu itatuondoa kwenye msingi na shabaha ya kujenga taifa letu kwani sisi ni wamoja na hatuwezi kubaguana kwa kiwango cha elimu na utajiri, kila mtu ana umuhimu na mchango wake katika kulitumikia taifa na sote tunategemeana.

Pamoja na changamoto zilizopo katika mfumo wa elimu nchini bado hakuondoi  umuhimu wa elimu na mchango mkubwa unaotolewa na wana taaluma nchini, niwapongeze wataalamu wetu wote kwa kazi nzuri wanayofanya na wasirudi nyuma.

Ili kumaliza changamoto zilizoko kwenye mfumo wa elimu Serikali ikubali kwa haraka kufanyia marekebisho kasoro zilizopo katika mfumo wa elimu. Pia ishirikishe wadau wa aina zote ili kupata sera, mtaala na sheria nzuri za kusimamia na kuendesha elimu nchini.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

 

 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: