Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira akisisitiza jambo akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo Bungeni Jijini Dodoma

Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira akisisitiza jambo akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo Bungeni Jijini Dodoma

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira ameitaka Wizara ya Kilimo iache kuimba wimbo wa Bei ya Mkulima badala yake watoke huko waende kwenye Pato la Mkulima ili kuongeza tija kubwa kwenye sekta hiyo.


Aliyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo ambapo Mbunge Neema alisema kwa kipindi kirefu Wizarani wamekuwa wakiongelea tu Bei ya Mkulima lakini wakati umefika sasa waongelee Pato la Mkulima kwa sababu wanapoongelea Pato la Mkulima lina faida mbili ya kwanza ni bei na ya pili ni wingi na ubora yaani kimahesabu Pato la Mkulima lina Variables mbili = Price/Bei x (Quantity/Wingi + Quality/Ubora). 

Alisema kwamba Wizara ya Kilimo wamekuwa wakiweka jitihada kwenye Bei ya Mkulima na sasa ameishauri Wizara ikumbuke hii Variable ya ya pili ya Q ambayo ni Quanity/Wingi na Quality/Ubora.

Mbunge Neema aliendelea kwa kusema kwamba kwa sababu Wabunge wengi wameongelea tija yetu ya kwenye kilimo anapenda kutoa mifano miwili: Kwa wenzetu wa Zambia wanauza kilo moja ya mahindi wanauza TZS. 250 mpaka 300 na wakiuza kwa bei hiyo wanarudisha gharama zao yaani wamefikia break-even point lakini kwetu sisi Tanzania ili kufikia kiwango cha break-even lazima tuuze kilo moja ya mahindi TZS.500 .

“Hivyo hivyo hata kwenye Pamba kwa nchi ambazo tunashindana nazo India, Brazili, China , Egypt wao wanazalisha eka moja kilo 1,000 hadi 1,250 na wao wakiingia sokoni wanaweza kuuza kwa bei ya TZS..500 kwa kilo na kwa kiwango hiko wamekuwa wamefikia kiwango cha break-even lakini sisi kwa sababu tija yetu ni ndogo tunazalisha eka hiyo hiyo moja kilo 250 hivyo hatuwezi kuuza kwa bei ya TZS 500 yaani mpaka ifike angalau TZS 1000” Alisema

Mbunge huyo alipendekeza kwamba ifika wakati Wizara ya Kilimo ianze kuongelea Pato la Mkulima na sio Bei ya Mkulima kwani kufanya hivyo wataweza kuongeza tija ambayo itaongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye Pato la Taifa kwa sababu wamekuwa wakisema asilimia 65 ya watanzania wapo kwenye Kilimo lakini bado Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 27 tu kwenye Pato la Taifa. 

Mbunge Lugangira alisisitiza kwamba kama Wizara itaendelea na Wimbo wa Bei ya Mkulima basi itakuwa inaendelea kufidia upungufu wetu wa tija kupitia Bei ya Mkulima jambo ambalo sio sahihi kwahiyo ni lazima sasa Wizara ya Kilimo ijikite katika Pato la Mkulima.

Hata hivyo pia Mbunge Lugangira aliishauri Wizara ya Kilimo ipitie upya Vituo vya Rasilimali ya Kilimo Ngazi ya Kata “Ward Agriculture Resource Centres” ione kama Vituo vinatumika kadiri ambavyo ilitakiwa na kama kuna  changamoto virudishwe kuwa chini ya Wizara ya Kilimo ili viweze kuchangia katika kukuza tija kubwa ya kilimo kama ilivyokusudiwa.

Kutokana na kwamba Vituo hivyo vilikuwepo kwa miaka mingi na Halmashauri zimekuwa hazitengi Bajeti ya Huduma ya Ugani jambo ambalo ni changamoto kubwa katika uendelezaji wa kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini.

“Kwanza nakushukuru sana Mh Spika kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti ya Wizara ya Kilimo na naomba nianza kwa kusema naunga mkono Hoja. Sera ya Kilimo hapa nchini inasema Mgani mmoja Kijiji kimoja kama tunavyofahamu kuna Vijiji takribani elfu 12000 na tuna Wagani elfu 7000 kwa sasa nchini hivyo tuna upungfu Wagani elfu  5000” Alisema

“Lakini pia napenda kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo hususani Waziri Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri wake Hussein Bashe kwa jitihada kubwa walizoweka kuleta Mageuzi kwenye Huduma za Ugani ikiwemo kutenga Bajeti kwa ajili ya kuwanulilia Maafisa Ugani vitendea kazi kama pikipiki, nawapongeza sana lakini bado kuna changamoto ambayo mimi ninaiona na kwamba bado Wizara ya Kilimo inategemea Afisa Ugani huyo awe mtaalamu kwa kila kitu ajue mazao yote, mbolea, wadudu,masuala ya madawa, fangazi, ukungu na nk jambo ambalo sio rahisi” Alisema

Mbunge Neema Lugangira alisema Serikali iliamua kuanzisha Vituo vya Rasilimali ya Kilimo Ngazi ya Kata ili viweze kuwa na tija kubwa kwenye kilimo na kama sikosei vituo hivyo vilianzishwa kwenye Kata 200 hapa nchini na pamoja na kuanzishwa Serikali iliweka wataalamu kwenye vituo hivyo, vitendea kazi kama kompyuta, Jenereta, screen za kufundishia nk,

“Katika hili niwapongeze Wizara ya Kilimo maana nimeskia kupitia Hotuba ya Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda kwamba wanakwenda kufufua Vituo hivyo lakini ningependa kushauri lazima Wizara ihakikishe Vituo hivyo viweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa kwa sababu hivi sasa Vituo hivyo vipo chini ya Halmashauri kwenye Halmashauri nyingi vituo hivyo havifanyi kazi iliyokusudiwa ya kuendeleza kilimo kwa mfano Kituo kilichopo Chamwino badala ya kufanya kazi ya kuendeleza kilimo inatumika na TARURA" Alisema.

Alisema pia hawawezi kuendeleza Kilimo wakati hizo Halmashauri ambazo karibia asilimia 70 ya Mapato yake ya Ndani yanatokana na Kilimo lakini Utengaji wa Bajeti ya Huduma ya Ugani hawatengi na kwakuwa suala hili linahusu Ofisi ya Rais TAMISEMI na Waziri yupo Bungeni anaskia  pengine atawaambia wanapanga vipi kuhakikisha hizo Halmashauri zinatenga Bajeti ya Huduma ya Ugani.

“Na mimi naamini lengo zima la kuanzishwa Vituo hivyo ilikuwa ni kuhakikisha wanaimarisha Huduma ya Ugani na wakifanya hivyo wataweza kuongeza tija na muhimu zaidi kuongeza Pato la Mkulima.

Mbunge Lugangira alimaliza kwa kusisitiza: "Kwa muda mrefu tumekuwa tukiongelea Bei la Mkulima na kabla sijaingia hapa Bungeni nilikuwa nafanya kazi kwenye Shirika ambalo lipo chini ya Wizara ya kilimo la SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania) kama Mkurugenzi wa Idara ya Sera na nimefurahi nimemuona bosi wangu Mr. Geoffrey Kirenga yupo kwenye Ukumbi wa Bunge kwa hiyo naendelea kusisitiza Wizara ya Kilimo iache Wimbo wa Bei ya Mkulima na ijikite katika Pato la Mkulima” Alisema


 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment:

Back To Top