MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina akizungumza
bungeni Dodoma wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2021/2022

 

 

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina ameibua tatizo kubwa la ukosefu wa zahanati nchini ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 6,197 havina huduma za afya hivyo wananchi kulazimika kutembea umbali wa wastani wa kilomita 10 hadi 20 kufuata huduma za afya katika vijiji jirani na hivyo kusababisha vifo kwa wajawazito na watoto wakihangaika kutafuta huduma umbali mrefu.

Mpina amesema hayo bungeni Dodoma wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2021/2022 na kuishauri Serikali kufanya maamuzi ya kuanza kupeleka kwanza waganga, wauguzi na dawa katika vijiji hivyo ili wananchi waanze kupata huduma wakati wakisubiri ujenzi wa majengo ya Zahanati ukamilike.

“Mh. Naibu Spika tunayoshida kubwa hapa nchini, kubwa kweli kweli ya upungufu mkubwa sana wa zahanati na kama tunavyofahamu huko ndiko kwenye msingi wa afya ya mwanzo lakini hapa nchini kwa takwimu tulizonazo toka Uhuru tumeweza kujenga zahanati 6,120 maana yake mpaka sasa hivi tuna upungufu wa zahanati 6,197 kwa hiyo tuna vijiji 6,197 havina zahanati kwa hiyo ni asilimia 50.3 ya wananchi hawa hawana huduma hiyo” amesema Mpina.

Mpina amesema hali hiyo imesababisha adha kubwa kwa wananchi wakiwemo akina mama wajawazito kwani hawawezi kujifungua mpaka watembee umbali wa wastani wa kilomita 10 mpaka 20 kutafuta  huduma hiyo kwenye vijiji jirani.

Hivyo watoto wadogo wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika kwenye huduma kutokana na umbali wa hizo kilomita kwenye vijiji jirani na suala limekuwa hilo  limekuwa likileta shida kubwa kwa wananchi hao kote nchini.

“Sasa hivi tumepiga hatua kubwa kwa mfano kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano ambapo sasa hivi tunapozungumza katika vizazi hai 1,000 wastani wa watoto 50 wanaopoteza maisha lakini pia katika wajawazito 100,000 akina mama 321 wanapoteza maisha sasa hizi takwimu pamoja na safari ndefu tuliyotoka tumeweza kuzipunguza lakini bado idadi hii ni kubwa na sababu yake kuwa kubwa ni upungufu wa hizi zahanati katika vijiji vyetu”amesema Mpina.

Mpina amesema magonjwa hayana likizo na wala hayana wikiendi lakini utaratibu uliopo sasa hivi wa Serikali ni kwamba zahanati mpaka ijengwe jengo kwanza na nyumba ya mganga iishe ndio sasa Serikali ifikirie kupeleka waganga na dawa jambo linaloleta madhara makubwa kwa wananchi.

“Hivi kuna shida gani leo hii tukaamua vijiji 6,197 ambavyo havina huduma ya afya tukapeleka daktari, tukapeleka muuguzi, tukapeleka na dawa watu wakaanza kutibiwa leo hii badala ya kusubiri jengo lijengwe mpaka likamilike ndio tupeleke huduma kwanini miundombinu itangulie badala ya huduma kutangulia” amehoji Mpina.

Mpina amesema zahanati hizi kwa awali zinaweza tu zikaanzishwa hata kwenye nyumba ya kupanga na wananchi wakaanza kupatiwa huduma badala ya kusubiri mpaka majengo sasa leo miaka 61 ya Uhuru wananchi wanasubiri majengo yakamilike ndio wapate huduma.

“Miaka 61 hakuna huduma ya msingi kwenye kijiji husika tunasubiri mpaka tujenge zahanati, tunasubiri nyumba ya mganga ikamilike, tunasubiri jengo la zahanati likamilike kwanini haya tunayaruhusu yafanyike Mh. Naibu Spika”alihoji Mpina.

Mpina alibainisha kuwa jambo la kusikitisha zaidi ni pale ambako  wananchi wameshamaliza kujenga majengo hayo lakini hakuna daktari wala huduma na zahanati hizo hazijaanza kufanya kazi licha ya wananchi kujitolea nguvu zao kujenga na Serikali kuwekeza fedha .

“Mimi ninayo mifano ya vijiji karibia nane kwenye jimbo langu ambavyo zahanati zimejengwa na zimekamilika zina nyumba ya mganga, kuna zahanati imekamilika lakini hakuna huduma leo miaka 8 ukienda Kijiji cha Semu, ukienda Mwageni, ukienda Mwagayi, ukienda Mwandu Itinje, ukienda Ikigijo, ukienda Tindabuligi, ukienda Malwilo zahanati zimejengwa zimekamilika lakini hakuna huduma sasa haya mambo kwanini tunayaruhusu mh Naibu Spika” amehoji Mpina

Hivyo Mpina akaishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI kuamua sasa kumaliza tatizo la wananchi hao wa vijiji 6,197 nchini kote kwa kuwapelekea madaktari, dawa, wauguzi ili waanze kupata huduma mara moja lakini pia mahala ambako zahanati zimejengwa na kukamilika watumishi waende, dawa zipelekwe ili huduma zianze kutolewa.

Hata hivyo pamoja na changamoto hizo zilizopo, Mpina amewashukuru watoa huduma za afya nchini kwa juhudi kubwa wanazofanya kuwatibu wananchi na kuwawezesha kurejea katika hali zao za kawaida na kujenga uchumi huku akipongeza hatua ya Serikali ya kuongeza Madaktari.

“Mh. Naibu Spika na mimi niungane na wenzangu kuwapongeza sana wauguzi wote na watoa huduma wote wa afya hapa nchini kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kutibu watu wetu na kuwapatia maisha mapya na niipongeze pia Serikali kwa hatua nzuri ilizozichukua kuongeza idadi ya madaktari lakini pia na kuhakikisha kwamba vifaa tiba pamoja na vitendanishi vinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini”. Amesema Mpina.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: