Viongozi wa Msikiti wa Kibaigwa wilayani Kongwa Dodoma wakimuombea Dua Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile (wa kwanza kulia) baada ya Mbunge huyo kutoa Sadaka ya Futari na kuahidi kushirikiana nao kuanza ujenzi wa jengo kubwa la Msikiti.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akishiriki pamoja Futari aliyoaiandaa kwa wananchi wa Eneo la Mji wa Kibaigwa wilayani Kongwa, Dodoma.
Wananchi wa Mji wa Kibaigwa wilayani Kongwa, Dodoma wakipata futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile.


Na Charles James,


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ametoa Sadaka ya Futari kwa wananchi wa eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa, Dodoma ambapo amewahakikishia pia kushirikiana nao katika kuanza ujenzi wa jengo kubwa la Msikiti wao.

Ditopile amewaomba pia waumini wa Dini ya Kiislamu kutumia mfungo huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake yeye pamoja na viongozi wengine.

Akizungumza mara baada ya kufuturu, Mbunge Ditopile amesema anafahamu kuwa kuna mpango wa kuanza ujenzi wa jengo kubwa la Msikiti huo wa Kibaigwa na kuahidi kushirikiana kwa pamoja katika kuanza ujenzi huo.


" Ninafahamu mnataka kuanza ujenzi wa jengo kubwa la Msikiti hapa Kibaigwa, niko tayari kushirikiana nanyi katika kufanikisha ujenzi wa nyumba hii ya Mwenyezi Mungu, tutaanza pamoja na Inshallah naamini tutafanikisha.

Niwaombe mniletee vielelezo vyote pamoja na ramani ya ujenzi, tunao viongozi wengi na wadau wakubwa ambao tutawafikia na watatusaidia kujenga nyumba hii ya Mwenyezi Mungu.

Nisisitize tu kuendelea kuiombea serikali yetu ya awamu ya sita ambayo inaongozwa na Rais wetu Samia na wote ni mashahidi namna alivyoanza na kasi kubwa ya kulitumikia Taifa hili akisisitiza kazi iendelee sambamba na kuhubiri Umoja na mshikamano kwa Nchi yetu," Amesema Ditopile.

Kwa upande wake Imamu wa Msikiti huo wa Kibaigwa, Sheikh Salum Salum amempongeza Mbunge Ditopile kwa moyo wake huo wa kujitolea Sadaka ya kufuturisha na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwa na moyo huo huo.

" Hili ni jambo kubwa umefanya na limeacha alama kubwa kwetu, ni somo kwa wote ambao wamejaliwa kipato na uwezo wa kufuturisha wenzao katika mfungo wa Ramadhan, huu ni upendo mkubwa.

Mtume Muhammad wakati akizungumza na Maswahaba wake aliwaambia mtu yeyote atakayeweza kuwashibisha watu katika futari kipindi cha Ramadhan basi amesamehewa madhambi yake yote, tukuahidi kuendelea kuiombea Nchi yetu, Rais wetu pamoja na nyinyie wabunge wetu," Amesema Sheikh Salum Salum

Share To:

Post A Comment: