Jackline Kuwanda,Mpwapwa .Dodoma
Kamati ya Wilaya ya ulinzi wa Wanawake na Watoto Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma imetembelea Gereza la Wanawake Wilayani humo na kuridhishwa na mwenendo wa huduma zinazotolewa kwa wanawake.
Baada ya kutembelea Gereza hilo leo Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Paul Sweya amesema wameridhishwa na Mazingira Mazuri katika Gereza na namna ambavyo wanawake wanahudumiwa hasa katika kupatiwa haki zao za Msingi kama wanawake.
"Tumeridhishwa na Mazingira kiukweli ni mazuri na hata mama anapokuwa hapa na Mtoto wake ameendelea kuhudumiwa vizuri,tumemkuta mahabusu mmoja na mfungwa mmoja ,huyu mfungwa aliyefungwa kama jamii yake ingemsaidia basi asingekuwa hapa ana watoto saba ambao wanaomtegemea na faini yake ilikuwa shilingi laki tatu tu,tunaona pia Gereza hili linawanawake wawili tu hii inamaana kuwa Elimu imetolewa zaidi" amesema Sweya
Dodoma News Blog imezungumza na Mrakibu Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza sehemu ya Wanawake Veronica Mwasalemba amesema mwanamke anapoingia gerezani husitiriwa vyema bila ya kumvunjiwa haki zake ambazo anastahili kuzipata kama Mwanamke .
"Mwanamke anapokuja hapa huwa tunamsitiri vizuri yeye pamoja na Mtoto kama yuko na Mtoto ,watu wengi huwa wanaogopa sana wanaposikia gerezani hii si sehemu ya kuogopa mtu anapokuja hapa anajifunza mambo mengi na hata wakitoka hapa huko wanapokwenda huwa wamebadilika kutokana na Mafunzo ambayo wameyapata hapa" amesema Veronica
Aidha Amesema anatamani kuona Gereza hilo linakuwa na Mazingira Mazuri zaidi lakini kutokana na Changamoto ya kutokuwepo kwa baadhi ya vitu ameiomba kamati hiyo Kusaidia Ili Gereza hilo la wanawake Ili Mazingira yawe mazuri zaidi
"Unaona hapa kuna magodoro tunatamani vitanda vikawepo Ili na wao wawe katika Mazingira Mazuri ,naimani kamati hii itasaidia "amesema Veronica
Amesema wanawake wanaofungwa huacha pengo kuwa katika familia kwani ukiangalia yeye ndiye aliyebeba majukumu mazito ya kuhudumia familia lakini linapokuja suala la kufungwa husababisha hata watoto aliyowaacha kuishi bila ya kuwa na uangalizi mzuri.
"Unakuta mama kafungwa huku akiacha watoto saba ,unajiuliza hawa watoto huko nje wataishije na kama unavyojua mama yeye ndiye kila kitu katika familia ,na hata ikifika wakati wa kujitetea Mahakamani wengi wao huwa wanaogopa anaulizwa unakipi cha kuiambia mahakama anasema hana akishatoka ukimuuliza anasema alikuwa anaogopa ,huenda angeiambia mahakama kuwa anawatoto kadhaa wanaomtegemea kungekuwa na njia rahisi ya kumsaidia " amesema Veronica
Kwa upande wa Hakimu Mkazi Wilayani humo Lusajo Mutua akizungumza na mtandao huu amesema jamii inaweza kukosa picha kwanini mwanamke amepata adhabu "mtu yuko Mahakamani anaulizwa kwanini mahakama isikupe adhabu hii ,yawezekana alipewa nafasi
ya kujitetea lakini kutokana na uelewa mdogo anashindwa kujitetea ,hapa ndipo watu wanakuja kuona kuwa mahakama haijafanya kazi yake lakini si Kweli ,sisi tunamjali mwanamke na tunatoa adhabu kwa mujibu wa Sheria " amesema Lusajo
Mmoja wa wanawake ambaye anatumikia kifungo Cha miezi minne gerezani Neema Mazengo(si jina lake halisi ) mwenye watoto saba amesema alifungwa kutokana na kupishana kauli na mama Mkwee wake hali iliyopelekea kufungwa kwa miezi hiyo.
"Nilipishana kauli na mama Mkwee wangu hivyo niliamriwa kulipa faini ya shilingi laki tatu au kutumikia kufungo Cha miezi minne , sababu ya kukosa pesa ilibinibidi kutumikia kufungo hicho ,baadàye mume wangu aliipata hiyo laki tatu alitaka kuja kunilipia nikamwambia alipie watoto ada shuleni Ili waendelee na masomo mimi nitumikie kifungo "amesema
Shirika la Jukwaa la utu wa mtoto wilayani humo Children's Dignity Forum CDF kwa ufadhili wa Comic Relief kupitia mradi wa Haki ya Binti wamewezesha kikao cha robo mwaka cha kamati hiyo ambayo imekuwa na msaada mkubwa katika kuwasiadia wanawake na watoto pindi wanapokumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya Vitendo vya ukatili dhidi yao.
Mwisho.
Post A Comment: