Katibu Mkuu Ndugu Daniel Chongolo amekutana na kuzungumza na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mzee Pius Msekwa katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu Lumumba na kumuahidi kukitumikia, kukisimamia na kukiimarisha zaidi Chama Cha Mapinduzi.
Chongolo amemhakikishia Mzee Msekwa kuwa Chama kipo salama chini ya Sekreterieti anayoiongoza na kwamba Katiba, Kanuni, taratibu na miongozo ya Chama iliyowekwa na Waasisi wa CCM itaendelea kuheshimiwa, kulindwa na kufuatwa, na kwamba Jahazi la CCM chini ya uongozi wake halitakwenda mrama.
Katibu Mkuu mpya wa CCM ameeleza kuwa mafunzo ya uongozi, utawala na siasa aliyoyapata wakati wote akiwa mtumishi kwenye Chama na Serikalini yamemkomaza na kumuandaa vyema kwa nafasi aliyoteuliwa na Mwenyekiti wa CCM Ndugu Samia Sukuhu Hassan. Chongolo amemueleza Mzee Msekwa kuwa amejifunza mengi kutoka kwa Wazee wastaafu aliobahatika kufanya kazi chini yao, amejifunza Ujasiri, kujiamini na kupata upeo na maarifa ya kutosha.
"Nakushukuru sana Mzee Msekwa, wewe na viongozi wenzako wastaafu kwa jinsi mlivyonilea. Nimechota maarifa na kujifunza mengi kutoka kwenu na kuniandaa. Nichukue nafasi hii kukuhakikishia kwa fikra zile zile, nidhamu ile ile na misimamo inayozingatia mabadiliko ya nyakati CCM kitaendelea kubaki chama bora Barani Afrika "Alisema Chongolo.
Ndugu Chongolo amesema licha ya kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha ataendelea kujifunza zaidi. Amesema kila atakapokwama hatosita kukimbilia kwao kwa ushauri na elimu ya uongozi.
Kwa upande wake Mzee Msekwa alisema CCM hakijawahi kumkabidhi mwanachama wake yeyote dhamana ya kuongoza hata ofisi ya tawi ikiwa mtu au mwanachama huyo hatoshi na hana vigezo. Hivyo akamuhakikishia Ndugu Chongolo kuwa Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wamejiridhisha kuwa anatosha, akamshauri aonyeshe utiifu, nidhamu na kukisimamia chama kwa uamunifu na kupokea na kuzingatia maelekezo atakayopewa na Mwenyekiti na Vikao vya Chama.
"Una wajibu wa kuhakikisha Sekreterieti yako muda wote mnakuwa na msimamo wa pamoja. Una kazi ya kutekeleza maagizo aidha ya H/kuu ya Taifa au ya Kamati Kuu ya CCM na kutekeleza" Alisema Mzee Msekwa.
#ChamaImara
#kaziIendelee
Post A Comment: