Na Angela Msimbira TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Ummy Mwalimu ameziagiza Sekretarieti za Mkoa kuhakikisha zinasimamia, kushauri na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa katika masuala mazima ya ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali
Akiongea kwenye kikao na viongozi wa Mkoa wa Dodoma leo, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria na miongozo, Sekretarieti ya Mikoa ndicho chombo cha kumshauri Mkuu wa Mkoa na kuzishauri Halmashauri katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa makusanyo na matumizi ya mapato ya Serikali.
Ameendelea kusema kuwa Sekretarieti za Mikoa nchini kuacha kufanyakazi kwa kutuma maelekezo kwa njia ya maandishi badala yake wahakikishe pia wanazitembelea Mamlaka za Serikali za Mitaa au kuziita Halmashauri husika kila baada ya miezi minne ili kujadiliana mipango ya maendeleo ambayo imepangwa kutekelezwa kwa muda huo.
“Naziagiza Sekretarieti za Mikoa zote nchini kuhakikisha wanafanya vikao mara nne kwa mwaka kwa kuziita Halmashauri husika ambazo zipo katika mikoa yao na kujadili mipango iliyopangwa kimkoa kwa kuangali kiasi cha mapato kilichokusanywa, matumizi yaliyofanyika na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini changamoto mbalimbali zinazozikabili Mamlaka za Serikali za Mitaa.” ameagiza Waziri Ummy
Waziri. Ummy amesema kuwa tegemeo lake katika kutekeleza majukumu ya Wizara ni kuhakikisha Sekretarieti za Mikoa zinatekeleza majukumu yake kikamilifu katika kusimamia na kufuatilia Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Hata hivyo, kuhusu Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Waziri Ummy ameagiza watumishi waliohusika au kudhibitika na ubadhilifu, uzembe au matumizi mabaya ya rasilimali za umma, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Vilevile, amezitaka Sekretarieti za Mikoa kujenga mahusiano mazuri katika utendaji kazi kwa kuheshimiana ,kufanya kazi kama timu ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi utakaoleta matokeo chanya.
Post A Comment: