Na. Angela Msimbira TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza watendaji wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri na baraza la madiwani ili kuweza kutimiza malengo ya serikali ya kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo wakati akiongea na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Jijini Dodoma mara baada ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hiyo
Amewataka wataalam kuhakikisha wanazingatia ushauri wa baraza la madiwani kwa kuchuja masuala ya muhimu na yanayoonekana yanaenda kinyume na sheria na taratibu wawashirikishe Wakuu wa Mikoa.
“Msiwadharau Madiwani na kudhani hawajasoma, wapo madiwani wanaelimu ya kutosha,hao ndio wawakilishi wa wananchi na wamechaguliwa na wananchi wapeni ushirikiano ili kuleta maendeleo katika Halmashauri zetu “amesema Waziri Ummy
Amefafanua kuwa madiwani ndio wawakilishi wa wananchi na wamechaguliwa kwa ajili ya kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili , hivyo ni vyema watendaji wa Halmashauri wakahakikisha wanaimarisha mahusiano katika utendaji kazi na baraza la madiwani ili kuleta mabadiliko na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Halmashauri.
Wakati huohuo Waziri Ummy amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya chamwino Athumani Masasi kujenga mahusiano mazuri na watumishi wa Halmashauri hiyo ili kuhakikisha wanaweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato kutokana na halmashauri hiyo kutokufanya vizuri katika ukusanyaji wa Mapato.
Aidha amemuagiza Mweka hazina wa Halmashauri hiyokuhakikisha anapeleka benki kiasi cha shilingi milioni 139 hadi kufikia tarehe 15/04/20201 fedha ambazo zilikusanywa lakini hazikuwekwa benki
Post A Comment: