Wasema ni uhakika wa Maisha yajayo
Wanafunzi wa Sayansi ya Madini ya vito kutoka kituo cha Jemolojia Tanzania kilichopo mkoani Arusha wamesema elimu wanayoipata kupitia kituo hicho inawapa uhakika wa Maisha yao ya baadae kutokana na kuwa na wigo mpana wa kujiajiri na hata kuajiriwa.
Akizungumza wakati wa mahojiano na wanahabari waliofika kituoni hapo mwanafunzi (Jina limehifadhiwa) alisema elimu anayoipata inasaidia katika kutambua na kuthaminisha aina za madini ya vito, itamsaidia kutambua madini halisi na madini feki na hivyo kutopata hasara endapo ataamua kujiingiza katika biashara ya madini.
Amesema elimu ya sayansi ya madini ya vito ina uwanja mpana wa kujiajiri ikiwa ni masuala ya ukataji, ung’arishaji na hata usonara hivyo anaona fursa pana pindi atakapoamua kujiajiri. Ameongezea kuwa elimu hii ina manufaa makubwa sana kwenye biashara ya madini.
Aidha, amewaasa watanzania hususani vijana kutokujihusisha na biashara ya madini ya vito pasipokuwa na uelewa wa kutambua na kuthaminisha madini hayo kwani kufanya hivyo kutapelekea kupata hasara na kupoteza mtaji kwani anaweza kuuziwa madini yasiyo halisi kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wafanyabiashara ya madini wasiokuwa waaminifu.
“Serikali imewekeza pesa nyingi kwenye kituo hiki ili kutusaidia kupata uwelewa wa madini ya vito, ni vema tutumie fursa hii kujitokeza kwa wingi kusoma kuliko kufanya biashara pasipokuwa na elimu hii muhimu” alisisitiza.
Akizungumzia manufaa anayoyapata kutokana na elimu ya sayansi ya madini ya vito Eva Mowo alisema kuwa yeye ni mwajiriwa kwenye Sekta ya Madini, elimu anayoipata itakwenda kuongezea nguvu miongoni mwa watumishi wengine wanaojikita katika suala zima la uthaminishaji na utambuzi wa madini ya vito.
Amewataka watanzania wengine wenye maono ya kujihusisha na biashara ya madini ya vito kujiandikisha katika kituo hicho ili wapate ujuzi.
Ameelezea kuwa chuo hicho kina mazingira rafiki ya kujifunza pamoja na vifaa vya kutosha vilivyowekezwa na serikali
Akizungumzia hatua zinazopitiwa katika suala zima la utambuzi na uthaminishaji madini ya Vito, mkufunzi Eusebi Bernard amesema utambuzi wa madini unapitia hatua ya Jemoliiia, refractometer, upimaji wa uzito (specific gravity) pamoja na hadubini hatua inayosaidia kutambua baina ya madini halisi na yaliyo feki au madini yanayotengenezwa viwandani.
Post A Comment: