Na Atley Kuni, DODOMA.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe amewataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha fedha zinazotengwa katika bajeti kwa ajili ya shughuli za afua za lishe zinatolewa ili kutokwamisha kazi hizo.
Akifungua kikao cha siku tatu leo tarehe 28 Aprili, 2021, mjini Dodoma, Prof. Shemdoe amesema kila mwaka serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kushughulikia masuala ya afua za Lishe, lakini tatizo hutokea wakati wa upangaji wa vipaumbele.
Amesema licha ya ongezeko la bajeti katika mamlaka za serikali za mitaa kutoka Sh. bilioni 11.6 mwaka 2017/18 hadi Sh.bilioni 16.87 2019/20 lakini kumekuwa na utoaji wa fedha za afua za lishe usio wa kuridhisha.
“Kuanzia sasa pamoja na vipimo vingine vya ufanisi vinavyotumika kuwapima Wakurugenzi, suala la afua za lishe kitakuwa ni kigezo muhimu katika kuwapima watendaji hao, hivyo lazima wahakikishe masula yote ya suala la Lishe yanapewa kipaumbele” amesema Prof. Shemdoe.
Pia, Katibu Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuzingatia miongozo inayotaka kutengwa Sh.1000 kwa kila mtoto aliye chini ya miaka mitano kwa ajili ya lishe.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Shemdoe hakusita kuwanyooshea vidole wadau wanaoshirikiana na Serikali kwa kuwataka kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa wanapotekeleza miradi yao na kutoa taarifa kila robo mwaka ikiwepo taarifa za fedha wanazopokea kutoka kwa wafadhili kuingizwa kwenye mipango ya Bajeti za Halmashauri.
“Tukifanya hivyo tutaepuka kupeleka fedha eneo moja na kufanya shughuli zile zile, bado kuna wadau wanafanya shughuli za lishe bila kuzingatia mkataba waliowekeana na uongozi, Mashirika yasiyo ya serikali yanayofanya shughuli za lishe wahakikishe wanashirikiana na TAMISEMI na mamlaka zingine zilizo chini ya Ofisi hiyo wakati wa utekelezaji,”alisema.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha katibu Mkuu kufungua Mkutano huo, Mratibu wa Lishe, TAMISEMI, Mwita Waibe, alisema tangu kuanzisha idara katika mamlaka za serikali za mitaa pamoja na mambo mengine wameanzisha mfumo wa (Information Management Monotoring and Evaluation System -IMES), ambao unafuatilia na kupata takwimu sahihi za afua za lishe.
Mwita alisema sekta ya lishe ina changamoto ya watumishi kwani katika mikoa 26 ni mikoa 20 tu yenye wataalamu wa lishe na kati ya halmashauri 184 ni halmashauri 66 pekee zenye wataalamu hao.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki 80 wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Maofisa Lishe nchini, Bibi, Bertha Donald ameiomba serikali kuhimiza utoaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya lishe katika halmashauri.
“Mtakumbuka Waziri wa Nchi Mhe. Ummy Mwalimu alinukuliwa akisema “Wakurugenzi wa halmashauri ambao halmashauri zao hazijafikia asilimia 50 ya ukusanyaji mapato hawatoshi,” Hivyo tungefurahi kusikia pia Wakurugenzi watakaoshindwa kutenga na kutoa kipaumbele kwenye fedha za Lishe hawatoshi”
Kikao hicho cha siku tatu, kitatumika Kujadili, uratibu na utekelezaji wa afua za lishe katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2020/21 sambamba na kuona mafanikio yaliyopatikana kisha kuweka mikakati endelevu kwenye sekta hiyo muhimu nchini.
Post A Comment: