Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Kulia), Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapwa wakibadilishana mawazo, mara baada ya Naibu Waziri Ulega kufika katika ofisi za mkuu wa mkoa huo kabla ya kuanza ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga.
NA. MWANDISHI WETU, MKINGA
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka wananchi wa Kijiji
cha Horohoro Kijijini Kata ya Duga katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga,
kutoruhusu mifugo ipitishwe kinyemela mpakani kwenda nchi jirani badala
yake wawafichue wanaofanya hivyo ili kuwadhibiti kwani serikali inakosa
mapato.
Ulega aliyasema
hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo
kwa kutembelea eneo lenye ekari 23 ambapo kutajengwa mnada wa mifugo
kijijini hapo na kusema kuwa mnada huo utakuwa chachu ya kuinua
maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema
lazima wananchi wilayani hapo kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa
kudhibiti mifugo kupitishwa kinyemela kwenda nje ya nchi ili kuiwezesha
serikali kukusanya mapato hatua ambayo itakuwa ni chachu kubwa kwao
kuwezesha maendeleo.
“Niwaambie
tu kwamba lazima hivi sasa tujipange kwa ujio wa fursa za mnada huu
kwani baada ya miaka miwili eneo hili litakuwa na picha tofauti na
ilivyokuwa hapo awali na litafungua ukurasa mpya wa maendelea kwenye
eneo lenu na tumekubaliana wizarani jambo hilo litaanza mwezi wa tano,
wazee wa duga mtupe ushirikiano kwa vijana wetu ambao watakuja kufanya
kazi hapa.“ Alisema Ulega
“RC
Shigella utakuwa umeacha alama kwa hili na nyinyi wananchi RC ametoa
rai mnada huo usigeuke kuwa ni dude ambalo litakuwa limekaa halina
shughuli za kufanya watu wanapitisha mifugo njia za panya na nyie
mnawaona na hamtoi taarifa kuzuia jambo hilo.” Alifafanua
Naibu
Waziri huyo alisema mnada huo ukianza kufanya kazi, eneo hilo litakuwa
na shughuli mbalimbali ambazo zitawasaidia kuwaingizia vipato mbalimbali
vya kimaendeleo hali ambayo itasaidia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja
na taifa kwa ujumla.
“Lakini
niwaambie kwamba mkiacha watu wanapitisha mifugo kwa njia ya panya
hakuna nchi inachokipata na wananchi hamuwezi kupata chochote hapo ni
sehemu nzuri ya kuhakikisha mnapaombea na kupiga dua, sala tuweze kuinua
uchumi wetu watu wa Mkinga.” Alisema
Aidha
alisema mnada huo utaanza mwezi Mei mwaka huu, huku akiwataka wakazi wa
eneo la Kata ya Duga kuwapa ushirikiano watumishi ambao watapelekwa kwa
ajili ya kufanya kazi hiyo ya kuhakikisha wanakusanya ushuru wa
serikali.
Aliwataka pia
wafugaji wa eneo hilo kuhakikisha wanafuga kisasa ili waweze kuwa na
ng’ombe wenye tija zaidi kutokana na kwamba watanzania wapo kwenye
mazingira mazuri ya kufuga kisasa tofauti na nchi nyingine.
“Mhe.
Rais wetu Samia Suluhu Hassan anataka kuona ng’ombe wenye kilo 500
diwani wa Kata ya Duga na wengine tunataka tukimbie mchakamchaka tufikie
lengo la Rais anataka kuona tunauza nyama inatupa tija, mfugaji
anabadilika anapata kipato na nchi inapata mapato ya kutosha.” Alisema
Naibu
Waziri huyo alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella
alibainisha kuwa mkoa unataka kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo
lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa ikiwa baadhi ya watu wanapitisha
ng’ombe kwenda nje ya nchi kinyemela kwa kutumia njia zisizo rasmi.
Alifafanua
kuwa ili kuongeza mapato ya serikali kupitia mifugo, katika mwaka ujao
wa fedha 2021/2022 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kutumia Shilingi
Bilioni 4 na Milioni 400 kwa ajili ya kujenga minada mbalimbali nchini
ukiwemo wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kata ya Duga katika Wilaya ya
Mkinga Mkoani Tanga.
Alisema
ujenzi huo unatokana na takwa la kisheria la magonjwa ya wanyama namba
17 ya mwaka 2003 ambayo inataka kufanyika hayo huku akieleza kuwa wizara
ina mipango mingi ya kuhakikisha wanawasaidia wafugaji kuhusu sehemu za
malisho.
Awali
akizungumza katika eneo hilo la mnada Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine
Shigella alisema moja ya tatizo kubwa lililopo eneo la mpakani ni
kutokuwa na mnada wa uhakika kwa ajili ya wafanyabiashara na wafugaji wa
mifugo, ndiyo maana serikali ya Mkoa wa Tanga na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi zinataka kusiwe na ufugaji wa kuhamahama.
Shigella
alisema hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni hivi karibuni, ameeleza nia yake ya
kutaka kuona wafugaji matajiri na siyo wa kuhamahama na ili kuweza
kujenga mazingira wezeshi ya eneo la kuuzia mifugo kwani bila kufanya
hivyo, wafanyabiashara wamekuwa wakienda kuwalangua wafugaji kwenye
mazizi yao na hivyo kujikuta hawanufaiki ipasavyo.
“Kuna
soko kubwa nchini Kenya ambapo baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara
wasiokuwa waaminifu walikuwa wanasafirisha mifugo kwenda Kenya na baadhi
ya watumishi wa serikali wasiokuwa waaminifu ndio walikuwa wanaongoza
mchakato huo wa kusafirisha mifugo bila kupitia kwenye taratibu mahususi
zilizopo.” Alisema Shigella
Hata
hivyo alisema anaishukuru wizara kwa kuliona hilo na kuunda kamati na
kuweza kubaini uwepo wa changamoto walizokuwa wanalalamikia
wafanyabiashara na wananchi wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kwani kubwa
walilokuwa nalo ni mifugo kupitishwa kwenye njia isiyokuwa rasmi,
kutokana na kutokuwa na eneo maalumu ambalo mifugo kabla haijasafirishwa
inatakiwa ipumzishwe mahali ambapo itakaguliwa magonjwa na kukusanywa
kwa tozo kabla ya kusafirishwa kwenda nchi jirani.
Kwa
upande wake Afisa Biashara wa Minada kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Bw. Basil Mataba alisema wizara ina jumla ya minada ya upili 14 na
minada 11 ya mpakani ambapo mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini mara
utakapoanza kufanya kazi utakuwa wa 12.
Bw.
Mataba alisema wanategemea Mwezi Mei mwaka huu mnada wa Kijiji cha
Horohoro Kijijini utaanza kufanya kazi hivyo kuondoa adha ambazo
walikuwa wakizipata wafanyabiashara na wafugaji kutorosha mifugo kwenda
nje ya nchi ili kuuza mifugo yao.
Alibainisha
hadi sasa eneo hilo la mnada tayari shughuli mbalimbali zinaendelea
ikiwemo ya kufyeka nyasi na tayari kibanda cha kukusanyia ushuru
kimeshasimikwa wakati wakiendelea na ujenzi wa eneo hilo huku akieleza
kwamba wizara itaendelea na hatua za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya uzio
wa awali.
Post A Comment: