Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mifugo iliyopo katika mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam huku akimuuliza mmoja wa wafanyabiashara wa mnada huo bei ya mifugo inayouzwa mnadani hapo. (Picha na Edward Kondela.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye fimbo) akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kusikiliza kero zao na kubainisha namna wizara ilivyojipanga kuziba maeneo yasiyo na uzio na kutatua kero za maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo. (Picha na Edward Kondela.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam amezungumza kwa njia ya simu na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, kuhusu uboreshaji wa barabara kutoka Gongo la Mboto hadi katika mnada huo, baada ya wafanyabiashara kulalamikia ubovu wa barabara hiyo hali inayoathiri mifugo yao. (Picha na Edward Kondela).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akipima kwa kutumia fimbo eneo ambalo linalalamikiwa na wafanyabiashara kuwa ni hatari kwa ng’ombe kupita kutokana na ardhi ya eneo hilo kuwa na maji mengi na udongo kuwa laini. Prof. Gabriel amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam. (Picha na Edward Kondela).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akiongea na Meneja Mnada wa Kimataifa wa Pugu Bw. Kerambo Samwel (wa kwanza kulia) na daktari mkuu wa mnada huo Dkt. Abdul Kyarumbika, wakati akimaliza zaiara yake katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu na kuwataka kuwa na utaratibu wa kutatua changamoto ndogokwa wakati ambazo zipo ndani ya uwezo wao. (Picha na Edward Kondela.


Na. Edward Kondela

Wafanyabiashara katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam, wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kutatua changamoto zilizopo katika mnada huo ili uwe na tija kwao na taifa kwa ujumla.

Wakizungumza jana (12.04.2021) baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabirel kufika mnadani hapo, kwa ajili ya kufuatilia maelekezo ya uboreshaji aliyoyatoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki baada ya kufika mnadani hapo hivi karibuni, wamesema wana imani kuwa mnada huo ukiboreshwa zaidi utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.

Baadhi ya wafanyabiashara waliowasilisha kero zao kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel wamesema bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ya uhakika kwa ajili ya kunyweshea mifugo yao, uzio wa mnada kutokuwepo katika baadhi ya maeneo na kuchangia mifugo kutoka nje ya mnada hali ambayo inaweza kusababisha baadhi ya mifugo kupotea.

“Tatizo kubwa hapa kwenye mnada huu ni maji kwa ajili ya mifugo viongozi mbalimbali wamewahi kuja hapa pamoja na kuchimba kisima na kuwekwa birika la kunywea maji mifugo, lakini hakujawahi kuwepo maji hata siku moja ninashauri lirekebishwe lambo ambalo limekuwa likitumiwa siku nyingi tutakuwa na uhakika wa maji.” Amesema Bw. Said Waziri mmoja wa wadau katika mnada huo.

Aidha, baadhi ya wafanyabiashara hao wamemuomba katibu mkuu huyo kuangalia uwezekano wa ukarabati wa barabara kutoka Gongo la Mboto ambayo inaelekea kwenye mnada huo ili magari yanayobeba mifugo yaweze kupita kwa urahisi kwa kuwa mifugo imekuwa ikipata majeraha na mingine kufa kutokana na kukanyagana wakati magari hayo yanapopita kwenye barabara hiyo ambayo ina mashimo makubwa.

Akizungumza mara baada ya kuwasikiliza wafanyabiashara hao Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara itafanya kila liwezekanalo ianze kufanya ukarabati wa uzio wa mnada kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/21 na kuendelea na ukarabati katika bajeti ijayo ya mwaka fedha 2021/22.

Prof. Gabriel amesema suala la uzio wizara inalipa kipaumbele likisimamiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ili mnada huo wa kimataifa wa Pugu uweze kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara wa mnada huo.

“Nikiri kwamba pamoja na mambo mengine alichonituma waziri kuja kuangalia kwa umakini sana ni suala la uzio na tutaona jinsi gani ya kuanza kwa mwaka huu wa fedha na tutalianza mara moja na nimeshawaelekeza wataalamu waje kuangalia nini cha kufanya.” Amesema Prof. Gabriel

Kuhusu changamoto ya ubovu wa barabara kutoka Gongo la Mboto hadi katika mnada huo, katibu mkuu huyo ameongea kwa njia ya simu akiwa mnadani hapo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, ambaye amesema atalisimamia suala hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Prof. Gabriel amesema kuhusu changamoto ya ukosefu wa maji, suala hilo analichukua kwa ajili ya kulifanyia kazi zaidi na kutafuta njia ambayo itaweza kusaidia uwepo wa maji ya uhakika kwa ajili ya kunyweshea mifugo.

Pia, katibu mkuu huyo ameelekeza kuanza kutumika mara moja kipakilio cha mifugo kwenye malori ambacho kimekamilika licha ya uwepo wa baadhi ya marekebisho ambayo ameelekeza yafanyiwe huku kikiendelea kutumika kutokana na wafanyabiashara kulalamika kupata wakati mgumu wakati wa kupakia na kushusha mifugo kwenye malori.

Kufuatia maelekezo hayo baadhi ya wafanyabiashara wamesema wamefurahishwa na kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na kubainisha kuwa wamepata imani kubwa kwa wizara hiyo kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki zaidi.

 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: