Tanzania Kupokea Uenyekiti wa ADPA


Uzalishaji wa Almasi nchini wafikia Carat  Laki 497 kwa mwaka


Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Dodoma


Tanzania inatarajia kubeba Ajenda ya  Kuanzishwa kwa Masoko ya Madini kwa   Nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika  mara baada ya kupokea Uenyekiti wa  Jumuiya hiyo lengo likiwa ni kuziwezesha nchi hizo kuuza madini yao  kwenye masoko ya ndani ikiwemo  kuyaongezea thamani .


Hayo yamebainishwa  Aprili 7 jijini Dodoma na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Saba (7) wa Mawaziri wa nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika ( African Diamonds Producers Association- ADPA) ambao unatanguliwa na mkutano wa Wataalam kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.


Ameeleza kuwa, faida ya Tanzania kuwa Mwenyekiti ya Jumuiya hiyo kutaipa nafasi ya kusukuma agenda muhimu zinazohusu sekta ya madini ikiwemo kuziita nchi hizo kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini.


Ameongeza kuwa, katika kipindi chake cha Uenyekiti kama nchi, itazishawishi nchi wanachama kuwa na mfumo wa Kisheria unaofanana ili kuziwesha  kunufaika na rasilimali madini ikiwemo kuzilinda.

‘’ Faida ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hii ni kuingiza mawazo yetu kwenye jamii kubwa. Tutatumia uzoefu wetu  kutangaza fursa za kibiashara kwenye sekta ya madini na lengo letu likiwa ni kuifanya Tanzania kuwa Hub ya  biashara ya madini kwa sababu tuna kila sababu ya kufanya hivyo,’’ amesema Waziri Biteko.


Akizungumzia hali ya sasa ya uzalishaji  wa madini ya almasi nchini, amesema kuwa, kama nchi inao Mgodi  mmoja mkubwa  wa Almasi wa  Williamson Diamond Limited (WDL)  uliopo  eneo la Mwadui Mkoani Shinyanga ambapo  uzalishaji wake  kwa mwaka umefikia Carat Laki 497 ukiwa ni uzalishaji mkubwa ukilinganishwa na uzalishaji mkubwa wa mwisho uliofanyika mwaka 1977 ambapo zilizalishwa Carat Laki 370.


‘’Kipindi cha janga la ugonjwa wa Corona bei ya almasi ilishuka na sehemu ya mgodi ilifanyiwa matengenezo. Hapa nchini, soko la almasi lipo mkoani Shinyanga na Dar es Salaam lakini soko la dunia liko Antwerp nchini Ubelgiji. Ukizungumzia mapato ya madini yanayoongoza ni dhahabu, inafuata almasi na madini ya ujenzi,’’ ameeleza Waziri Biteko.


Mgodi wa Almasi wa WDL ni mgodi wa ubia ambapo Serikali inamiliki hisa asilimia 25 na Kampuni ya Wilcroft inamiliki asilimia 75. 


Aidha, akizungumzia mkutano huo amesema kuwa, mbali na majadiliano, nchi wanachama watapata fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusiana na usimamizi wa sekta ya madini, kuimarisha utendaji  katika wizara ikiwemo kuhakikisha mifumo ya ADPA inaboreshwa ili kuwa na manufaa ya nchi wanachama.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya amesema kwa kuwa nchi ya Tanzania ni sehemu ya nchi wazalishaji wa madini ya almasi  Afrika wanayo fursa ya kushiriki mikutano hiyo.


Tanzania ndiye  Mwenyeji wa Mkutano  wa mwaka huu wa  Siku Mbili  unaofanyika tarehe 7 na 8 Aprili, 2021, kwa njia ya Video Conference. Jumuiya hiyo inajumuisha jumla ya nchi wanachama 19 kati yao 12 zikiwa nchi wanachama na 7 nchi waangalizi. Nchi wanachama ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea na Sierra Leone.  Nchi waangalizi ni pamoja na Algeria, Jamhuri ya Congo, Cote D’ivore, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania.


Jumuiya hiyo ilianzishwa mwaka 2006 kwa mujibu wa Azimio la Luanda Angola na Sheria za ADPA, lengo ilikuwa ni kuzipatia nchi zinazozalisha madini ya almasi Afrika jukwaa la kuzikutanisha katika kusudi moja la kuhakikisha rasilimali madini zinanuifaisha nchi wanachama. Aidha, kupitia jukwaa hilo  nchi zinapata fursa  za kubadilishana taarifa za uzoefu katika sekta ya madini na kujenga uwezo wa wataalam kuhusiana na masuala ya almasi. Vilevile, kupitia jukwaa hilo, nchi zinaweza kuleta masilahi ya nchi wanachama kuhusiana na biashara ya almasi duniani.


Tanzania inatarajia kupokea kijiti cha Uanachama wa Jumuiya hiyo kutoka nchi ya Jamhuri ya Namibia ambapo Balozi wa Namibia nchini ataikabidhi Tanzania uenyekiti huo, jijini Dodoma.


xxxxxxxxxxx


*CAPTIONS*


1. Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na Wanahabari  wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) unaofanyika  kwa Njia ya Video tarehe 7 Aprili, 2021 Jijini Dodoma


2. Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Doto Biteko (Kulia), Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (Kushoto) wakizungumza na Wanahabari  wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) unaofanyika  kwa Njia ya Video arehe 7 Aprili, 2021 Jijini Dodoma


3. Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akifuatilia mkutano kwa njia ya Video wa Mawaziri wa Nchi za Afrika zinazozalisha Madini ya Almasi tarehe 7 Aprili, 2021 unaofanyika Jijini Dodoma


4. Picha ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila na Wataalam wa Madini katika Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) unaofanyika  kwa Njia ya Video tarehe 7 Aprili, 2021 Jijini Dodoma

Share To:

msumbanews

Post A Comment: