Wanawake wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida kutoka katika vikundi vinne vya Mfuu, Mrumba, Wajifya na Misenga wakitandaza mabomba juzi katika shamba lao la  kilimo cha mbogamboga baada ya kuwezeshwa na Asasi ya TAHA.
Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari (kulia) akiwaelekeza jambo wanawake hao wakati wa kuandaa shamba hilo.
Wanawake hao wakishiriki kuchimba mifereji kwa ajili ya kutandaza mabomba ya mfumo wa umwagiliaji katika shamba hilo.
Muonekano wa shamba hilo.
Wanawake wakishiriki kubeba mabomba kupeleka shambani.
Wanawake hao wakishiriki kuunganisha mabomba kabla ya kutandazwa shambani.


Na  Dotto Mwaibale, Singida 


WANAWAKE wa Kata za Sepuka na Irisya wilayani  Ikungi mkoani Singida wameanza kuandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na  matunda baada ya kuwezeshwa na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.

Wamefikia hatua hiyo baada ya kupatiwa mafunzo na Asasi hiyo kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa ni kujikomboa kiuchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi wakati wakiandaa shamba hilo lililopo Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka kwa ajili ya kilimo hicho baadhi ya wanawake hao kutoka katika vikundi vinne vya Mfuu, Mrumba, Wajifya na Misenga walitoa pongezi kwa asasi hiyo na halmashauri hiyo kwa kuwathamini kwa kuwapelekea mradi huo.

Katibu wa Kikundi cha Mrumba, Asia Gudo alisema mradi huo wameupokea kwa mikono miwili na kuwa wamefurahi kwani  wanatarajia kunufaika kiuchumi na mazao watakayopata ambayo ameyataja kuwa ni nyanya, pilipili hoho na miche ya miembe watakapoyauza  fedha zitakazo patikana watawasomesha watoto wao, kununua mifugo na kujikimu kimaisha.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Mfuu, Mwahija Njiku alisema kupitia mradi huo waliowezeshwa na UN-WOMEN na TAHA utawakomboa kiuchumi na kuwapunguzia mzigo wanaume katika majukumu ya kulea familia.

Kwa upande wake Mayasa Omari ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Wajifya aliipongeza asasi hiyo ya TAHA kwa kuwapelekea mradi huo ambao ni endelevu na kuwa utawakomboa wanawake kwa namna moja hama nyingine.

Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari alisema hivi sasa kwa kushirikiana na wanawake hao wapo katika hatua ya kufunga mifumo ya umwagiliaji katika mashamba manne na kuwa wamefikia hatua nzuri.

Alitaja mazao watakayoyapanda katika mashamba hayo kuwa ni nyanya maji, pilipili kichaa pamoja na vitunguu.

" Mazao haya yamekuwa zaidi ya moja kwenye eneo moja kwa sababu tutayatumia kama mashamba darasa ambapo wakulima watakuja kujifunza ili nao wapeleke teknolojia hiyo maeneo mengine.  

Bakari alisema kwa kuwa kilimo hicho ni kipya katika wilaya hiyo mwitikio wa wanawake hao ni mkubwa huku wakiwa na hamu ya kuona matokeo yake baada ya kupanda mazao hayo.

Asasi ya TAHA yenye makao yake makuu jijini Arusha inafanya kazi zake na kuendesha mradi kama huo  katika mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja ( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba ( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) ,Ikungi-Singida na  Shinyanga.

Share To:

Post A Comment: