Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu Lissu, akizungumza katika kikao kazi cha Kamati ya Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ngazi ya mkoa (MTAKUWWA) kilichoketi jana mkoani hapa.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Hinza ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa katika kikao hicho na viongozi wengine. Kutoka kulia ni Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Joshua Ntandu Lisu na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Shukran Mbago.
Wajumbe wa MTAKUWWA wakiwa kwenye kikao hicho.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Shukuru Mbago, akizungumzia majukumu ya Mtakuwwa. kwenye kikao hicho.
Mratibu wa mradi kutoka shirika hilo , Annamaria Mashaka akitoa mada katika kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Mwezeshaji kutoka ESTL, Hawa Hussein akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Kata ya Kisaki wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkazi wa Kata ya Kisaki Debora James akichangia jambo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkutano ukiendelea.
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Singida, Tumaini Christopha, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Na Dotto Mwaibale,Singida.
SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland limewakutanisha kwa pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya mkoa kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.
Wajumbe hao ambao ni viongozi wa sekta na idara mbalimbali za serikali, Ngo's,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu na mwenyekiti wake ambaye ni katibu tawala mkoa wamekutana jana kwenye kikao kazi kujadili mbinu za kukabiliana na ukatili.
Kamati hiyo pamoja na mambo mengine imetoka na mapendekezo kadhaa ikiwemo kuiomba serikali kuanzisha mitaala ya elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye shule,na kuitaka sekretarieti ya kamati hiyo kuandaa utaratibu mzuri wa utoaji elimu ya ukatili kwa sekta na idara za serikali ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ukatili.
Aidha wajumbe hao wameiomba serikali kutenga fedha ili kugharamikia vipimo vya vinasaba (DNA) inapotokea kesi za ukatili na kuhitajika vipimo kama ilivyo kwa sampuli zingine kwani mara nyingi hatua hizo zinashindwa kuchukuliwa kutokana na gharama.
Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Joshua Ntandu Lisu aliomba ushirikiano zaidi kwenye kamati hiyo ili hatua za kukabiliana na ukatili ziendelee kusonga mbele na lengo hasa ni kupinga ukatili.
"Sisi kama shirika tutaendelea kuiwezesha kamati hii ya MTAKUWWA ili tuendelee kusonga mbele katika harakati za kupinga ukatili."alisema Lisu.
Wakati huo huo ESTL pia ilikutana na wananchi wa Kata ya Kisaki Manispaa ya Singida na kufanyanao mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu ya ukatili na kutanabaisha madhara yatokanayo na ukatili hususani ukeketaji ambapo awali kabla ya mkutano huo shirika hilo liliendesha mafunzo kwa makundi ya vijana, viongozi wa dini na mangariba wastaafu pamoja na watu maarufu katika kata hiyo.
Post A Comment: