OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Ummy Mwalimu amesema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itatekeleza mikakati mahsusi ya kuimarisha ubora wa elimu Sekondari ikiwemo kuongeza kiwango cha ufaulu wa somo la hesabu.
Waziri Ummy ameyasema hayo Leo katika uzinduzi wa Program ya 'Kiu Hisabati Ubungo', iliyoandaliwa na Mbunge wa Ubungo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof.Kitila Mkumbo.
Program hiyo inalenga kuchochea kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Shule za Sekondari za Jimbo la Ubungo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Ummy amesema wanafunzi wengi hawafaulu somo la hesabu ambapo katika matokeo ya Mitihani ya kidato Cha nne mwaka 2020 yanaonyesha kuwa wanafunzi waliofaulu somo la hesabu ni asilimia 20 tu.
"Yaani ni wanafunzi 20 tu kati ya wanafunzi 100 waliofaulu somo la Hesabu ambapo waliopata A ni 0.7%, B - 1.3%, C - 6.8%; D -11.3% na F - 79.9%," amesema.
Amempongeza Prof.Mkumbo kwa kuanzisha program hiyo na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi kufanya vizuri katika somo la hesabu.
"Kwa upande wetu, Serikali ya Awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan itatekeleza mikakati mahususi ya kuimarisha ubora wa Elimu ikiwemo kuongeza kiwango cha ufaulu wa somo la hesabu kwa kufanya mafunzo kazini kwa walimu wote wa hesabu kuhusu mbinu bora za ufundishaji darasani na jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wa uelewa mdogo,"amesema
Pia amesema kuchapisha na kusambaza vitabu vya hesabu kwa wanafunzi wote
wa sekondari ili kila mwanafunzi awe na kitabu chake kitakachomsaidia wakati wa muda wa ziada kufanya mazoezi ya hesabu
"Kufufua na kuanzisha Vituo vya Kujifunzia vya Walimu (Teachers Resource Centres) katika Tarafa na kata ili walimu wajifunze mada ngumu kutoka kwa walimu mahiri na kuhamasisha wanafunzi kupenda hesabu kupitia klub za wanafunzi mashuleni," amesema
Kwa upande wake, Prof.Mkumbo ameahidi kutoa motisha kwa walimu wa Shule za Sekondari Ubungo ya sh.100,000 kwa kila daraja A ya Hesabu itakayopatikana.
Aidha ameahidi kulipia ada ya kidato Cha tano kwa wanafunzi wote wa Jimbo la Ubungo watakaopata daraja A ya Hesabu katika Mitihani ya kidato Cha nne
Post A Comment: