Na Mbaraka Kambona, Kigoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu wa kuendesha oparesheni za muda mfupi.
Ndaki alisema hayo wakati akizungumza na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma jana.
Akizungumza na wavuvi hao Ndaki alisema kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa.
“Tunataka kuja na mkakati endelevu wa namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki.
“Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu kisichokubalika”.
Kwa Mujibu wa Ndaki anasema walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika.
‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki.
Kuhusu baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama wahalifu wengine.
Aliongeza kuwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao.
Ndaki alisema kuwa hatalegeza
nati hasa linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa
ngazi zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza
kuwafichua wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.
Post A Comment: