Mkuu wa Mkoa Wa Singida Dk Rehema Nchimbi akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa wafanyabiashara yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) mjini hapa.
Maafisa kutoka Brela wakimkaribisha Mkuu wa mkoa kwa ajili ya kufungua mafunzo hayo. Wa pili kutoka kushoto ni Msaidizi wa Ofisi Mwandamizi Utawala kutoka Brela, Saada Kilabula na kulia ni Afisa Tehama kutoka Brela Hillary Mwendo.
Mkutano ukiendelea.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa wamesimama kwa dakika moja kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Mkutano ukiendelea.
Na Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameutaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) kutoa semina ya biashara kwa viongozi wa Serikali na dini ili kuwa na uelewa kutokana na wao kukutana na watu wengi jambo litakalosaidia wananchi kuwa na uelewa wanapofanya biashara zao.
Dkt. Nchimbi alitoa kauli hiyo leo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yanayotolewa na wakala huo kwa wafanyabiashara mkoani hapa yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa RC Mission.
Alisema wananchi wanachokihitaji sio kuifahamu Brela bali kupata matokeo chanya kwenye biashara zao kupitia Brela,hivyo anategemea kuona mabadiliko makubwa baada ya mafunzo hayo.
"Niwaombe njooni mtoe Semina kwa watendaji wa Serikali na Viongozi wa dini hawa wanawatu wengi wakielewa hawa mtakuwa mmefundisha wengi,tuko tayari kutenga muda hata masaa mawili ili mtupe hii elimu."
Aidha Dkt. Nchimbi aliutaka wakala huo kuendesha kwa haraka zoezi la usajili wa biashara na leseni kutokana na sasa kutumia teknolojia inayokwenda kwa haraka ili kuondoa usumbufu wa kufuatilia mara kwa mara mfanyabiashara, huku akiwataka wafanyabiashara kufuata taratibu, maadili na nidhamu katika biashara.
"Nawapongeza Brela kwa ubunifu huu wa kutoa mafunzo ya kuwaelimisha wafanyabiashara ili kuelewa namna ya ufanyaji biashara yatatoa fursa kwa maendeleo ya nchi.Utumishi ni kuwafuata wananchi hongereni sana." alisema Dk Nchimbi na kuongeza.
"Haya mafunzo yatatujengea uelewa,kuelewa sisi wote ni wamoja,tuko kwenye mnyororo mmoja,akiharibu mmoja ameharibu mfumo wote wa kibiashara.Biashara inahitaji nidhamu,umakini maadili na bidii." alisema Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake Msaidizi wa ofisi Mwandamizi Utawala kutoka Brela Saada Kilabula alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa wananchi ambapo yameanza hapa Singida na baadaye Dodoma na kuhitimishwa mkoani Morogoro kwa awamu hii ambapo pia zoezi hilo kwa baadaye linatarajiwa kufanyika hadi ngazi za Wilaya na lengo hasa wananchi wawe na uelewa wa kibiashara.
Brela iliona kuna haja ya kutoa mafunzo hayo kwa wananchi kutokana na baadhi ya watu wasiowaaminifu kuwatoza fedha nyingi wananchi wanapohitaji kusajili biashara zao hivyo kupitia mafunzo hayo yataondoa huo usumbufu na kutambulisha mfumo wa namna ya kujasili biashara kupitia simu za mkononi.
"Hatujawahi kutoa mafunzo haya lakini tuliona kuna haja ya kuja huku chini kwa wananchi tuwape elimu kutokana na wengi kutozwa fedha nyingi wanaposajili biashara zao na baadhi ya watu wasiowaaminifu." alisema Kilabula.
Post A Comment: