Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano na kuwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais, Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza kupigania maendeleo ya Tanzania.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina ametumia hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwashukia vikali kikundi cha watu wanaojiita wakosoaji wanaobeza na kukashifu mafanikio ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano wakidai ilijaa ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mpina amehoji ni fisadi gani anayeweza kuongeza mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali, kudhibiti rushwa na ufisadi na kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40 na kuwezesha kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa fedha zetu za ndani sambamba na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Mpina amehoji fisadi gani atenge na kutoa kiasi cha shilingi trilioni 1.01 kugharamia elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari, kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka bilioni 348.7 mwaka 2015 hadi bilioni 450 mwaka 2020. Hatua ambayo imewezesha watoto wa masikini na wanyonge kupata fursa elimu bila shida yoyote tofauti na miaka ya nyuma ambapo watoto wa masikini walikosa fursa hiyo
Mpina ameuliza ni fisadi gani ambaye anaweza kuongeza bajeti ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka sh. Bilioni 31 mwaka 2015 hadi sh. Bilioni 270 mwaka 2020.
“Ni fisadi gani wa kununua vifaa vya kisasa, kusomesha madaktari bingwa hali iliyopelekea kuwezesha na kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini kwa magonjwa ya moyo, figo, mifupa na ubongo ambapo imesaidia kupunguza idadi ya rufaa kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95. Leo huduma hizi zinapatikana hapa nchini ambapo huko nyuma watu wengi walipoteza maisha kwa kukosa huduma”alihoji Mpina.
Pia Mpina ameuliza ni fisadi gani anayeweza kufungua njia zote za mawasiliano tangu akiwa Waziri na baadae Rais ambapo barabara za lami zimetandazwa kila sehemu, madaraja makubwa ya kimkakati yamejengwa, meli na reli mpya kujengwa na zilizokufa kufufuliwa, Ndege mpya 11 zimenunuliwa na viwanja vya ndege kujengwa sehemu nyingi ambapo imewawezesha watanzania kufika na kutamba kila kona ndani na nje ya nchi.
“Ni fisadi gani anayeweza kusambaza umeme kila kijiji ambapo vijiji vilivyopata umeme vimeongezeka kutoka 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwaka 2020, kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere ambao unagharimu trilioni 6.5 ambao utawezesha nchi yetu kuzalisha umeme wa Megawati 2115 wa bei nafuu” aliongeza Mpina.
Mpina amebainisha kuwa ni fisadi gani afute mikataba ya kifisadi mingi iliyokuwa ikilinyonya taifa mfano IPTL, Aggreko na Symbion ambayo ilikuwa ikiligharimu taifa bilioni 719 kwa mwaka leo fedha hizi zinatumiwa kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi.
“Ni fisadi gani aliyeweza kuumaliza ufisadi wenyewe, rushwa, ujangili, ujambazi, uvuvi haramu, madawa ya kulevya, mauaji ya vikongwe na albino, ajali za barabarani, aliyekomesha dhuluma kwa wananchi wanyonge”.alihoji.
Hivyo Mpina amesema tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi Mbabe wa Vita Mtetezi wa Wanyonge, kipenzi cha wengi Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa wema wake usiomithilika na kwa jinsi alivyopigana kiume kupambania maendeleo ya nchi yake.
“Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyesema kuwa ni nadra sana kupata viongozi wa aina ya Dk. Magufuli”alisema Mpina.
Mpina ameongeza kuwa tumeshuhudia pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa maarufu kama Baraza la 75 lililokamilisha mkutano wake maalum uliolenga kumkumbuka na kumuenzi Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo Umoja huo umetambua uwezo na jitihada alizokuwanazo JPM za kupambana na Rushwa na Ufisadi.
Pia kuboresha huduma, kujenga miradi mikubwa ya maendeleo na mageuzi makubwa ya uchumi kwa muda mfupi ambao umepelekea Tanzania kuingia uchumi wa kati katika kipindi kifupi cha miaka 5 badala ya miaka 10 iliyotarajiwa. Umoja huo wa Mataifa umetambua kuwa JPM aliwapenda sana Watanzania na aliipenda nchi yake.
Aidha Mpina amesema tunakumbuka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliamua kupeperusha bendera zake nusu mlingoti tarehe 26.03.2021 siku ya mazishi ya Dk. Magufuli ambapo pia tulishuhudia zaidi ya watu bilioni 4 duniani kote wakifuatilia tukio la mazishi yake.
“Hiyo ni heshima kubwa sana kwetu watanzania na duniani kwa ujumla kwa kuwa si kila kiongozi anapofariki kwa nafasi ya urais anapewa heshima hiyo kama aliyopewa Hayati Rais Magufuli”alisema.
Pia Mpina amepongeza Rais, Samia Suluhu Hassan Mwanamke Shupavu na Jasiri kwa uamuzi wake wa kukubali kuendesha kongamano maalum la kitaifa la viongozi wa dini kama sehemu ya kuendelea kuenzi na kutambua mchango Hayati Dk. John Pombe Magufuli uamuzi huu umegusa sana mioyo ya watanzania.
“Ndio maana nina kila sababu ya kusema wale wanaotumia kila aina ya mbinu kufuta ‘legacy’ ya Dk. Magufuli ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu, watanzania wanamfahamu JPM kwa namna alivyoyagusa maisha yao, hivyo wenye chuki binafsi waache mara moja na badala yake tuungane na Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza mafanikio na kulijenga taifa letu. Ninajua Mungu wetu wa mbinguni kamwe hatatuacha”amesema Mpina.
Hata hivyo Mpina amesema pamoja na mafanikio mengi tuliyoyapata kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato ameshauri Serikali kufanya tathmini ya vyanzo vya mapato ili kuibua fursa mpya na kuondoa changamoto zinazokwaza ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya Serikali.
Pia ameshauri Wizara na taasisi zenye vyanzo vya mapato ziwasilishe fursa na changamoto zilizopo katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kabla ya kusomwa Bajeti ya Serikali na Finance Bill kwa nia ya kuongeza wigo wa kukusanya kodi na kuondoa changamoto zilizopo.
Mpina pia ameshauri Serikali ikubali kuwekeza fedha katika miradi na maeneo yanayoweza kuongeza mapato ya Serikali kwa muda mfupi na kuendelea kuimarisha usimamizi kwa mujibu wa sheria.
Post A Comment: