*Mpina amvaa CAG, ahoji kwanini sababu ya hasara ya bilioni 60 ATCL haikutajwa aomba Kamati ya PAC kumbana zaidi ili ukweli ujulikane*
 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina ametilia shaka ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa namna ilivyoripoti hasara ya sh. bilioni 60 kwenye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kusababisha mkanganyiko mkubwa kwa wananchi.

Mpina amesema kwa mujibu wa Taarifa ya CAG inaonesha kuwa Kampuni ya ATCL ilipata hasara ya sh. bilioni 60 mwaka (2019/20), sh. bilioni 23 (2018/19) na kwamba sababu ya hasara hiyo iliyotajwa na CAG ni matumizi yanayohusisha usafirishaji wa abiria na mizigo kuongezeka kwa asilimia 45 kutoka sh. bilioni 133.6 mwaka 2018/2019 hadi kufikia sh. bilioni 193.6 mwaka 2019/2020.

Pia ripoti hiyo ilieleza mapato yaliongezeka kwa asilimia 41 kutoka sh. bilioni 116 hadi sh. bilioni 157.6 lakini cha kushangaza sababu za kuongezeka kwa matumizi hayo hazikuwekwa kwenye ripoti ya CAG licha ya kuwa zinafahamika wazi na kusababisha mkanganyiko mkubwa kwa wananchi.

Mpina amesema sababu hizo ni pamoja na kutokea mlipuko wa Covid-19 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 na kuathiri usafiri wa anga ambapo hapa nchini ndege zilikuwa zinafanya kazi kwa asilimia 20 tu.

Kampuni ya Air Tanzania iko kwenye mageuzi makubwa ambapo katika mwaka 2019/2020 ndege mpya 2 aina ya Boeing na Bomberdear zilinunuliwa na ndege zingine zilinunuliwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2018/2019 na hivyo kupelekea gharama za uendeshaji na utunzaji kuongezeka.

Pia ndege zinazotumiwa na Shirika la  Air Tanzania zimekodiwa kwa Wakala wa Ndege za Serikali na hivyo Kampuni inalazimika kulipa gharama ya ukodishaji kwa wakala huyo.

Kutokana na kuongezeka kwa ndege Shirika limelazimika kuajiri marubani na watumishi wengine ili kukidhi mahitaji ya utoaji huduma .

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 Shirika liliongeza kituo kipya cha nchini cha Mpanda na kufungua kituo nje ya nchi cha Mumbai India, Pia shirika liliongeza miruko katika  vituo vya Dodoma, Mwanza na Kilimanjaro.

Pia Kampuni ya ATCL ina deni la miaka ya nyuma la sh. bilioni 217 ambapo inalazimika kulipa riba kila mwaka  na mwaka huu wa 2019/20 shirika limelipa riba ya deni sh. bilioni 12.5 ikilinganishwa na malipo ya riba ya sh. bilioni 8 ya mwaka 2018/2019.
Kampuni ya ATCL imeanza mageuzi ya uwekezaji miaka miwili tu iliyopita na hivyo sio rahisi kupata faida leo.

Pia amewatoa wasiwasi wananchi kuwa Kampuni yetu ya ATCL inazidi kuimarika na kuwataka wanaobeza kwa namna moja au nyingine waache na badala yake wapende vitu na mafanikio ya nchi yao.

Mpina amebainisha ushahidi wa kampuni yetu kuimarika na mafanikio yaliyopatikana kwani kabla ya hatua hizi kuchukuliwa na Serikali ya awamu ya tano  shirika lilikuwa halina uwezo wa kulipa watumishi wake mishahara hivyo Serikali ililazimika kulipa mishahara yote kwa 100% lakini tunapozungumza leo Shirika letu linajitegemea kulipa mishahara ya watumishi wake kwa 87%.

Katika kipindi cha ukaguzi shirika lilikuwa na ukwasi wa bilioni 17.5 huu ni ushahidi kuwa kampuni yetu inaendelea vizuri
Kampuni imeajiri marubani waliofikia 80 na wote ni wazawa wakiwemo marubani wanawake ambao wote tunawaona wakirusha ndege zetu kwa umahiri mkubwa.

Pia kwa kufanya ulinganifu na makampuni mengine ya kigeni  mfano Kenya Airways (KQ) ambapo Kampuni ya KQ toka mwaka 1977 inaendelea kupata hasara kila mwaka lakini Serikali yake inaendelea kuwapa fedha za kuendesha shirika hilo kwa kutambua kuwa faida za usafiri wa anga ni mtambuka.

Kuongezaka kwa idadi ya watalii nchini ni ushahidi mwingine wa mafanikio ya shirika letu ambapo watalii wameongezeka kutoka milioni 1.1 (2015) hadi milioni 1.5 (2019) na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 (2015) hadi Dola za Marekani bilioni 2.6 (2019).

Huduma za biashara na uwekezaji nchini zimekuwa na ufanisi mkubwa najua watanzania hawajasahau abiria, bidhaa na mizigo yote kutoka nchini kwetu ilitegemea ndege za nje mfano. Mbogamboga, Maua, Samaki, Mabondo, Nyama kwenda masoko ya nje najua hatujasahau na hatutasahau.

Faida nyingine ni kuwahisha wagonjwa kupata matibabu ndani na nje ya nchi kwa gharama ndogo baada ya kununua ndege zetu mfano zamani mgonjwa alitakiwa kupelekwa India lazima apitie kwanza Dubai kuunganisha ndege za India kwa gharama kubwa na kutumia muda mrefu lakini baada ya kununua ndege zetu na kuanzisha ruti ya India gharama ya usafiri imepungua kwa asilimia 40 na muda umepungua kwa kiwango kikubwa na hivyo kuwahi kwenye huduma.

Kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Shirika la ndege Tanzania ni Mpina ameshauri watanzania wenzetu wanaobeza Kampuni yetu ya ATCL waache mara moja.

Pia Serikali ilipe deni la nyuma la ATCL la sh bilioni 217, Serikali iendelee kuwekeza kwa kuongeza idadi ya ndege za abiria na mizigo, kupanua na kujenga viwanja vipya vya ndege, kuongeza safari, marubani na kukarabati miundombinu muhimu mingine muhimu hii ni pamoja na  ujenzi wa uwanja mpya wa ndege Mkoa wa Simiyu.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: