Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas (kushoto) akizungumza leo katika kikao cha Mawaziri wa Wizara hiyo na Wizara ya Mawasiliano naTeknolojiaya Habari cha kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Sekta hizo yakisera, kisheria na kikanuni kwenye masuala ya mawasiliano nchini kilichofanyika jijini Dodoma.Kulia ni Katibu Mkuu waWizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula. Kikao hicho kimefanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mheshimiwa SamiaSuluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yakutaka kufanyika marekebisho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia Vyombo vya Habari hapa nchini hususani Televishen Mtandao (Online TV)
Na John Mapepele, Dodoma
Waziri anayesimamia Sekta ya Habari Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri anayesimamia Sekta ya Mawasiliano Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na timu ya Makatibu Wakuu na Wataalam wa Wizara hizo wamekaa na kujadili hoja mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za kisekta kufuatia maelekezo ya hivi karibuni ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maelekezo hayo aliyatoa wakati wa kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi ya kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia Vyombo vya Habari hususan Televisheni Mtandao (Online TV).
Majadiliano hayo yamefanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021 na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kwenye hoja 13 zilizoainishwa na Wizara hizo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo katika maeneo yote yenye mapungufu ili ziendane na hali halisi ya sasa na kuweka mifumo rafiki ya kushughulikia masuala yote yanayohusu sekta ya Mawasiliano na Utangazaji
“Tumeagiza Wataalam wafanye uchambuzi wa Kanuni za Maudhui Mtandaoni ili kuona kama zinaendana na mazingira ya sasa” amesisitiza Waziri Bashungwa
Ameongeza kuwa Wizara zimeaazimia kuja na mkakati wa kuwaelimisha wadau wa Sekta hizo ili kudhibiti makosa ya kimaudhui yanayofanywa na Vyombo vya Habari badala ya hali ilivyo sasa inayotoa adhabu kali zinazojikita kwenye utozaji wa faini kubwa pamoja na kufungiwa.
Suala lingine ambalo limeazimiwa kufanyiwa kazi ni chaneli za bure kutoonekana kwenye visimbusi ambavyo kimsingi zinapaswa kuonekana hata pale kifurushi kinapokuwa kimeisha muda wake.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kukua kwa teknolojia kumewezesha kukua kwa matumizi ya huduma za mawasiliano yakiwemo ya utangazaji hivyo katika kipindi kifupi kijacho Serikali kupitia Wizara hizo mbili itafanya maboresho makubwa kwenye kanuni husika ili kuendana na hali halisi ya sasa.
Ameongeza kuwa Serikali ilitunga Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali zikiwemo Sheria ya huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016, Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 na Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambazo pamoja na mambo mengine zinaelekeza kuweka mazingira wezeshi ya kukuza maudhui ya ndani (Local content).
Post A Comment: