Mbunge wa jimbo la Vunjo Mhe Dkt Charles Stephen Kimei amewashukuru wadau mbalimbali kuendelea kumuunga mkono katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi jimboni humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kivuko cha Mshiri kilichojengwa kwa ushirikiano wa wadau wa maendeleo wanaotoka kijiji cha Mshiri, wananchi wenyewe, diwani wa kata ya Marangu Mashariki Mhe Jonas Mawala pamoja na yeye mwenyewe Dkt Kimei amesema anaona fahari kuona namna wanavunjo wanavyoguswa na maendeleo ya jimbo lao hata kuwa tayari kufuatilia yanayoendelea na kushirikiana naye kama Mbunge na mtumishi wao kutatua changamoto zilizopo.
"Naomba sote tuone fahari ya kushiriki maendeleo ya jimbo letu, tusiiachie serikali pekee yake, na ninyi wananchi wa Mshiri mmeonesha mfano wa kuigwa hongereni sana.
Ushirikiano wetu huu umefanikisha kukamilika kwa ujenzi wa kivuko hiki ambacho ni imara na bora zaidi ambacho kitawaepusha watoto wetu, wazee wetu, mama zetu na vijana wetu na taabu ya kuvuka kwenye kivuko cha miti ambacho kilihatarisha sana usalama na hata uhai wao. Leo vyombo vya moto (pikipiki na magari) vitapita hapa tofauti na kile kivuko cha miti.
Hivyo niseme kwa ushirikiano huu naiona Vunjo Mpya yenye maendeleo makubwa ambayo sote tunaitamani." Alisema Dkt Kimei
Amewashukuru viongozi wa kijiji hicho cha Mshiri pamoja na diwani wa kata ya Marangu Mashariki Mhe Jonas Mawala kwa ubunifu na uaminifu walionao ambao ndio unawapa hamasa wadau kujitokeza kushiriki shughuli za maendeleo.
Post A Comment: