Mkazi wa Mtaa wa Kazaroho, Kata ya Mbugani katika Manispaa ya Tabora, Salumu Madinda amepoteza maisha papo hapo baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akichomelea sehemu iliyopasuka kwenye bodi la gari kwa kutumia mtambo wa kuchomelea (welding machine).
Baadhi ya watoto wa marehemu ambao walikuwa naye katika kiwanda chake kidogo cha uchomeleaji muda mfupi kabla ya kupatwa na umauti wake wameeleza namna tukio lilivyotokea wakati baba yao akiwa kazini.
"Mzee amefariki kutokana na shoti ya umeme chanzo kikubwa ni kuvuja kwa mashine, ilikuwa inavujisha voltage kwa wingi zaidi lakini zile waya mbili zakuchomea zilikuwa zimelala kwenye ardhi ambayo ilikuwa mbichi na ina unyevunyevu," amesema Juma Salumu, mtoto wa marehemu.
"Mzee alikuwa akichomolea gari aina ya Canter alikuwa amevaa viatu virefu kwa ajili ya usalama wa shoti ya umeme kama kawaida inavyotakiwa lakini kwa bahati mbaya ule unyevu wa chini ya ardhi alipopiga magoti ndipo shoti ilipompiga na kupelekea umauti wake," amesema Said Salumu, mtoto wa marehemu.
Muda mfupi baada ya mazishi kufanyika akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa huo, Rabani Daudi amesema Jeshi la Polisi lilifika na kujiridhisha juu ya tukio hilo na kuto ruksa ya mwili huo kuzikwa huku akiwaasa mafundi umeme na wananchi wote kuchua tahadhari kazini.
Chanzo- EATV
Post A Comment: