Serikali imetumia zaidi ya Sh milioni 600 kuboresha majengo ya Chuo cha Ualimu Singachini kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni muendelezo wa dhamira yake ya kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi za Elimu yanaboreshwa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ziara yake Mkoani humo kukagua mradi wa ukarabati katika Chuo Cha Ualimu Singachini.
Waziri Ndalichako amesema ameridhishwa na ukarabati uliofanyika ambapo pia wameweza kuongeza majengo mapya kwa kutumia fedha walizopatiwa.
Ukarabati katika Chuo hicho umetekelezwa kwa kutumia utaratibu wa "Force Account" kwa Usimamizi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo Waziri Ndalichako amewapongeza kwa usimamizi mzuri wa ukarabati wa Chuo hicho.
“Hiki chuo kimefanya zaidi ya ukarabati kwa sababu kuna majengo mapya ambayo yamejengwa ambayo ni bweni, jengo la utawala na vyumba viwili vya madarasa kwa ujumla mandhari ni nzuri, kwa kweli namshukuru Mhe. Rais kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu kuanzia kugharamia elimu bila malipo lakini pia kutoa fedha za kufanya ukarabati katika Taasisi za Elimu,” alisema Waziri Ndalichako.
Amesema Wizara anayoisimamia itaendelea kuhakikisha miundombinu ya elimu inaimarishwa na kuongeza fursa za elimu ili kuandaa walimu bora.
Ameahidi kuanza kazi ya ukarabati wa makazi ya walimu na wakufunzi kwani katika awamu ya kwanza ya maboresho ya Chuo yalijikita katika miundo mbinu ya ufundishaji na ujifunzaji.
“Tunafahamu kwamba katika awamu ya kwanza hadi ya tatu ya ukarabati tulijikita zaidi katika majengo ambayo yanatumiwa na watu wengi kama mabweni madarasa, kumbi za mikutano, na ofisi za walimu, sasa ni wakati muafaka wa kuwakumbuka watumishi kwa kuwa nazo zimechakaa,”alisema Waziri Ndalichako
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amewataka Wakufunzi katika Chuo cha Ualimu Singachini kuhuhakikisha wanahimiza suala la uzalendo na kujiandaa kuanza kutoa mafunzo ya ufundishaji somo jipya la Histotiria ya Tanzania.
Aidha amesema walimu wana mchango mkubwa katika kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kati kupitia Viwanda inatekelezwa kwa kutoa wanafunzi bora ambao wataendelea kuwa wataalamu wa fani mbalimbali katika sekta ambazo zinachagia kujenga uchumi wa nchi.
Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Singachini Cornelius Gasper amesema ukarabati na ujenzi wa majengo mapya katika Chuo hicho umetumia Force Account kama ilivyoelekezwa na ameishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwani maboresho hayo yameongeza morali ya wakufunzi kufanya kazi na wanafunzi kujifunza kwa bidii.
Post A Comment: