Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini inatarajia kukusanya shilingi bilioni 650 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 na kuendelea kuboresha shughuli za uchimbaji na madini ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi

 

Hayo yameelezwa leo tarehe 30 Machi, 2021 mjini Morogoro na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo alipokuwa akifungua kikao kazi kilichokutanisha wahasibu kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwenye  usimamizi wa mifumo ya fedha pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi.

 

Alisema kuwa, ili kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka wa fedha 2021-2022 linafikiwa kwa wakati, Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuongeza mikakati kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini, usimamizi zaidi kwenye masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha vitendea kazi vya kutosha vinakuwepo kwenye ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa na masoko ya madini.

 

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka wa fedha 2020-2021, Tarimo alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Februari, 2021 Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 399 ikiwa ni sawa na asilimia 113.7 ya lengo la kipindi husika ambalo lilikuwa ni kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 351.

 

Katika hatua nyingine, Tarimo aliwataka wahasibu kuendelea kuwa wabunifu kwenye utendaji kazi na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuli ili kuhakikisha kuwa Sekta inazidi kukua na kufikia mwaka 2025 inakuwa na mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa.

 

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya alisema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwapa wahasibu uelewa wa pamoja kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa  kutumia mifumo mbalimbali.

 

Mtinya alieleza maeneo mengine yanayoangaziwa katika kikao hicho kuwa ni pamoja na kujadili taarifa za utekelezaji wa ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa, usimamizi wa fedha za umma, sheria ya fedha za umma, uandaaji wa taarifa mbalimbali za kifedha na kuweka maazimio yatakayosaidia kutoa taarifa sahihi  na kuwezesha menejimenti kufanya maamuzi yenye tija.

 

Share To:

msumbanews

Post A Comment: