Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia moja ya barakoa iliyoshonwa na wanafunzi katika Chuo cha Maendeleo ya wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani kilimanjaro.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia wanafunzi wa fani ya Uashi katika Chuo cha Maendeleo ya wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani kilimanjaro wakijifunza kwa vitendo.
Muonekano wa moja ya majengo ya Chuo cha Maendeleo wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro baada ya ukarabati.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kwa kusimamia vizuri ukarabati wa majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga (FDC) kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro.


Waziri Ndalichako ametoa pongezi hizo mara baada ya kukagua ukarabati wa majengo katika Chuo hicho ambapo amesema ameridhishwa na ubora kazi iliyofanyika na kuwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa Serikali yao inawajali na imeboresha mazingira ya kujifunzia.


Amesema Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga ni moja kati ya Vyuo 54 vilivyofanyiwa ukarabati kupitia Mradi wa Mukuza Ujuzi na Stadi za Kazi unaosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Akizungumzia masuala ya nidhamu kwa wanafunzi, Waziri Ndalichako amewataka walimu pamoja na kufundisha masomo ya darasani  kuhakikisha  mafunzo juu ya uraia na uzalendo yanakuwa endelevu ili kuwa na vijana wenye nidhamu na  wazalendo  wanaothamini tunu zilizoachwa na waasisi wa nchi hii.  

  

“Hii kazi nzuri ambayo tumeifanya hapa muienzi na vifaa ambavyo mmeomba  naahidi kuwa nitavifanyia kazi, itakuwa  haina maana yoyote kama ninyi mtakuwa hamna uzalendo kwa sababu vifaa vinaweza vikaja na mkaviaharibu ni lazima vijana mlinde rasilimali za nchi yenu,”alisema Waziri Ndalichako.


Amewapongeza wanafunzi wa fani ya uashi katika Chuo hicho kwa kujenga jengo la  mlinzi na kusistiza kuwa hayo ndio mafunzo yanayotakiwa kwa kuwa vijana wanamaliza wakiwa na ujuzi


“Mafunzo na mitaala yetu ni mizuri lakini wakati mwingine vijana mnakuwa hamzingatii na kufuatilia kwa ukaribu masomo, kwa hiyo walimu niwasii kama ambavyo nimeona kazi nzuri mmeifanya muendelee kuwafundisha vijana wetu na msisahau kuwajengea maadili mema kwa ajili ya taifa letu,”amesisitiza  Waziri Ndalichako 


Waziri Ndalichako ameahidi kufanyia kazi changamoto za baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ili wanafunzi waweze kusoma vizuri.


Nae Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga Miriam Msomvu amesema ukarabati uliofanyika umetumia zaidi ya Sh milioni 560 na kwamba umewezesha kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 130 mwaka 2019 kufikia wanafunzi 312 mwaka 2021.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga wameishukuru Serikali kwa kufanya ukarabati mkubwa katika Chuo chao na kumuaomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwaondolea changamoto ya upungufu wa baadhi ya vifaa vya kujifunzia.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: