Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka Kamati ya Kitaifa kuwasilisha mpango kazi wake wa utekelezaji wa majukumu kwenye usimamizi wa ufungaji wa migodi nchini ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinafungwa pasipo kuathiri mazingira.


Waziri Biteko ametoa kauli hiyo mapema leo tarehe 04 Machi, 2021 kwenye kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma lengo likiwa ni kupokea taarifa ya majukumu yake kwenye usimamizi wa ufungaji wa migodi nchini.


"Ni vyema nikapata picha kamili ya mpango mzima wa majukumu yenu kwenye usimamizi wa ufungaji migodi pamoja na kutoa ushauri kwangu kabla ya kuidhinisha hati fungani za kampuni za madini zinazowasilisha mipango ya ufungaji wa migodi yake," amesema Waziri Biteko.


Katika hatua nyingine ameitaka kamati hiyo kujiridhisha gharama halisi za ufungaji migodi kwa kurudishia mazingira katika hali nzuri kabla ya kumshauri kuidhinisha hati fungani na kupitisha mipango ya ufungaji migodi. 


Aidha, Waziri Biteko amesema kuwa Serikali inapenda kuona Sekta ya Madini inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi bila kuathiri mazingira ya wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyopo kwenye machimbo ya madini.


"Haileti maana Serikali inaingiza mabilioni ya shilingi kutokana na Sekta ya Madini, huku wananchi wakiathirika hasa baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini," amesema Waziri Biteko.


Naye Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya mbali na kuipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri ameitaka  kuongeza kasi ya utendaji kwenye usimamizi wa mipango ya ufungaji migodi.


Kamati hiyo ina wajumbe kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Maji, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya  Mkemia Mkuu wa Serikali.


Wengine wanatoka katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: