Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akitoa salamu zake kwa waumini wa Masjid Rahman Kisauni, alipojumuika nao katika sala ya Ijumaa
WAZAZI na walezi wameshauriwa kurejesha mila na desturi katika Utamaduni wa kulea watoto kwa pamoja, ili kupunguza vitendo vya udhalilishaji nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Sulieman Abdulla alitoa ushauri huo wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Rahman Kisauni Wilaya ya Magharibi “B” alipojumuika nao katika ibada ya Sala ya Ijumaa.
Alisema Zanzibar ya zamani haikuwa na vitendo vya udhalilishaji kutokana na malezi waliyokuwa nayo wazee, jambo ambalo kwa sasa limepotea katika jamii zetu hivyo amewataka wazee na walezi kurudisha utamaduni huo, ili kuisaidia Serikali katika malezi na kupunguza wimbi la udhalilishaji.
“Mfumo wa malezi waliokuwa nao wazee wetu zamani ulikuwa mzuri sana kwani uliruhusu motto kulelewa kwa mashirikiano ya pamoja” Alisema Mhe. Hemed
Mheshimiwa Hemed alisema wazazi wana jukumu la kufatilia nyendo za watoto wao, kwa kuhakikisha wanashiriki vyema katika masomo ya ziada, kwa kuwasimia wanapokwenda na kurudi hasa nyaki za usiku, kitendo ambacho kitasaidia zaidi kupunguza vitendo hivyo.
Makamu wa Pili wa Rais aliendelea kuwasisitiza wananchi wa Zanzibar kuzidi kuishauri Serikali yao kwa kutoa maoni na mapendekezo, kwani Serikali ya Awamu ya Nane inahitaji zaidi maoni ya wananchi wake, akitolea mfano kutumia mtandao uliozindulliwa hivi karibuni wa sema na Rais Mwinyi.
“Mfumo huu aliouzindua Dk. Hussein Mwinyi umekusudia kuwashirikisha wananchi wengi kutoa maoni yao”
Akizungumia juu ya suala la umoja na mshikamano, Mhe. Hemed amewataka wazanzibari kuendeleza jambo hilo ambalo litapelekea kujenga Zanzibar yenye maendeleo, hasa katika kuwasaidia vijana kupata ajira za uhakika.
Mheshimiwa Hemed aliwasihi waumini hao kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini, kwani bila ya amani hapatokuwa na maendeleo, akiongeza kuwa nchi inapokuwa na amani hata wawekezaji watavutika na kuja kuwekeza kwa maslahi ya Taifa.
Nae Khatibu aliehutubu katika Msikiti huo Abasi Jumbe Sheha alisema kuwa ni wajibu wa waumini na wananchi kwa ujumla kuwa watiifu na wasikivu kwa viongozi wao, huku akiwataka waumini hao kutambua kuwa uongozi ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kumpa amtakae.
Pamoja na mambo mengine, sheikh Abasi aliwataka waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kuzidisha Ibada ili kujijengea mustakbali mzuri wa maisha yao ya kesho akhera.
Kassim Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Post A Comment: