N
WANANCHI wanaomiliki ardhi katika kijiji cha Kiseriani kata ya Mlangarini, halmashauri ya wilaya ya Arusha, mkoani Arusha wamejitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya urasimishaji unaofanyika katika maeneo yao, wakati wa utekelezaji wa mradi wa urasimishaji Ardhi katika kijiji hicho, mradi unaotekelezwa kupitia wataamu wake wa ndani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari jana, walipotembelea eneo la Kiserian, wamiliki hao wa ardhi, wamekiri kuchangamkia fursa hiyo, na kudai imekuja wakati muafaka na kupongeza juhudi za halmashauri hiyo, kwa kutekeleza mradi wa urasimishaji ardhi katika kijiji cha Kiseriani na vitongoji vyake, zoezi lililoshirikisha wananchi wote katika hatua zote.
Katibu wa kamati ya Urasimishaji Kitongoji cha Losirwai, Lomayan Maiko Mollel, ameweka wazi kuwa wananchi wa Kiseriani, wameupokea mradi wa urasimishaji kwa matumaini makubwa ndio maana wamejitokeza kwa wingi, kurasimisha maeneo yao waliyokuwa wanayamiliki kihalali lakini bila ya kuwa na vibali halali vinavyoatambulika kisheria, kutokana na maeneo hayo kutokuwa yamepimwa wala kuwa na ramani ya mipango miji pamoja na gharama kubwa za urasimihsaji zilizokuwa zinatozwa hapo awali.
"Kiukweli wananchi wa Kiseriani wamefuhishwa na kuridhishwa na urasimishaji wa maeneo yao kutokana na kufanyika kwa gharama nafuu tangu zoezi linaze katika kitongoji changu tuu, cha Losirwai zaidi ya watu 150 wameshalipia na wengine wanaendelea kulipa na baada ya kulipia tuu, watalamu wanaweka bicon bila kuchelewa, kupitia zoezi hilo wananchi wamepata imani kubwa na serikali yao, naweza sema tumepagawa." amesisitiza Katibu huyo.
Hata hivyo wananchi hao, wamekiri kupata muamko mkubwa kutokana na elimu waliyopewa na watalamu pamoja na gharama nafuu za urasimishaji kwa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakimilki maeneo yao bila vibali maalumu vya serikali kutokana na kushindwa kumudu gharama zilizokuwa zinatozwa na kuongeza kwamba zoezi hilo limekuja wakati muafaka, wakiamaini litasaidia kuondoa migogoro ya ardhi iliyokuwa inajitokeza kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na watu wasio waaminifu na kwa kuchukulia kigezo cha uelewa mdogo wa watu wengi.
Rick Nkya mmiliki wa eneo kitongoji cha Losirwai na Longiva amesema kuwa, ushirikishwaji uliotolewa na watalamu wa Ardhi, umefanya wananchi kuwa na uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa mipango miji, na kuongeza kuwa kuna athari kubwa za kuishi kwenye maeneo yasiyopangwa, maeneo ambayo hakuna miundombinu ya kueleweka huku wananchi wakijenga nyumba zao bila mpangilio, lakini huku Kiseriani kila mwenye kiwanja amekubali kutoa mita tano mpaka 6 kwa ajili ya barabara za ndani ya mitaa.
"Binafsi ninaishi Sakina, wakati nikinunua kiwanja hakukuwa kumepimwa wala kupangwa, kila mtu amejenga anavyojisikia, jambo ambalo limeasababisha, ukosefu wa miundo mbinu ya barabara, mpaka sasa kila mtu ana kinjia cha kufika nyumbani kwake tu na baadhi ya watu hawana kabisha njia, jambo linalosababisha migogoro mingi miongoni mwa majirani, hata hivyo gharama zake ni nafuu"amefafanua Nkya.
Naye Mratibu wa Urasimishaji, halmashauri ya wilaya ya Arusha na afisa mipango miji, Faiz Mnaro amesema kuwa, tayari wananchi wamepata elimu ya Urasimishaji, na wamejitokeza kufanya utambuzi na upimaji wa maeneo yao, pamoja na kukubaliana uwepo wa miundombinu ya barabara katika maeneo yao, na kuongeza kuwa kutokana na upimaji kila mtaa utakuwa na barabara za kuanzia Mita 5 - 6, huku barabara za kuunganisha vijiji na miji zitakuwa na upana wa kuanzia Mita 8 - 15.
Aidha Mnaro, ameelezea faida za urasimishaji ni pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi, kumiliki ardhi kisheria ukiwa na kumbukubu halali na hatimaye kupata hati, ardhi inapanda thamani ikiwa imepangwa na kupimwa, inainua maisha ya watu kwa kuweza kupata mikopo na pia kama dhamana kwa lolote zaidi shughuli za maendeleo zinafanyika kwa kasi katika maeneo yaliyopimwa, na kufafanua kuwa urasimishaji ni zoezi kutambua maeneo na mipaka inafuata kupima, na kupata hati miliki.
Halmashauri ya wilaya ya Arusha inaendelea na zoezi la urasimishaji katika kijiji cha Kiseriani katika vitongoji vya Kiseriani, Longiva na Losurwai, ambapo jumla ya viwanja 3,051 vimetambuliwa na vinatarajiwa kupimwa na kurasimishwa kwa kuandaa ramani ya Mipango Miji pamoja na wamiliki hao kupatiwa hati miliki.
Post A Comment: