Wahasibu Tume ya Madini wametakiwa kuendelea kutoa ushauri katika masuala ya kifedha kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini na kuiwezesha kufikia lengo lake la kuchangia kwa asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo tarehe 31 Machi, 2021 mjini Morogoro na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku tatu kilichoshirikisha wahasibu wa Tume ya Madini kutoka Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kilichoanza mapema tarehe 29 Machi, 2021.
" Napenda niwakumbushe kuwa, Tume ya Madini inawategemea sana katika utoaji wa ushauri wa kitaalam katika masuala yote yanayohusu fedha, utawala pamoja na ununuzi ambayo mmekuwa mkiyafanya kwa ufanisi katika maeneo yenu," alisema Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba aliwapongeza wahasibu kwa jitihada kubwa katika kuhakikisha maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo kwa kuzingatia maslahi ya umma.
Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka wa fedha 2020-2021, Mhandisi Samamba alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Machi, 2021 Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 445.3 ikiwa ni sawa na asilimia 84.5 ya lengo la mwaka ambalo lilikuwa ni kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 526.7.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba aliwataka wahasibu kuendelea kuwa wabunifu kwenye utendaji kazi na kusisitiza kuwa Tume ya Madini itaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuli ili kuhakikisha kuwa Sekta inazidi kukua na kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Wakati huo huo aliwahakikishia wachimbaji wadogo kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kuwasaidia kwa kuwatengea maeneo ya uchimbaji wa madini na kuwaunganisha na Taasisi za Kifedha na kupatiwa mikopo.
"Nimekuwa nikipokea simu nyingi kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini wakihofia hatma ya shughuli zao baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli lakini niwahahakishie kwa uwepo wa uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula Tume ya Madini itaendelea kusimamia kwa nguvu zake maslahi ya wachimbaji wadogo hivyo waendelee kujiamini na kufanya uzalishaji wa manufaa ya nchi.
Katika kikao kazi hicho masuala yaliyoangaziwa ni pamoja na kujadili taarifa za utekelezaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, usimamizi wa fedha za umma, sheria ya fedha za umma, uandaaji wa taarifa mbalimbali za kifedha na kuweka maazimio yatakayosaidia kutoa taarifa sahihi na kuwezesha menejimenti kufanya maamuzi yenye tija kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Post A Comment: