Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika ambapo amewapa siku tano kuhakikisha wanaiondoa mifugo yao wanayoitunza kwenye mnada huo ikisubiri kwenda kuchinjwa. (16.03.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na watendaji wa mnada wa kizota, viongozi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma na viongozi kutoka WMUV wakati alipotembelea mnada Kizota kukagua shughuli zinazofanyika ambapo ameagiza ujenzi wa ukuta katika mnada huo uanze haraka. (16.03.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akikagua miundombinu iliyopo katika Mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika. (16.03.2021)
Wafanyabiashara wa mifugo katika Mnada wa Kizota Jijini Dodoma wametakiwa kuacha kuhifadhi mifugo yao inayokwenda machinjioni katika eneo la mnada kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul leo (16.03.2021) wakati alipotembelea mnada huo kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika ambapo pia alikutana na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo.
Gekul amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa zipo taratibu za uendeshaji wa Minada ya Upili ambapo mifugo ikishanunuliwa inatakiwa kuchukuliwa na sio kutuzwa hapo ikisubiri kupelekwa machinjioni.
“Hivyo natoa siku tano kwa wafanyabiashara wote ambao mnatunza mifugo yenu hapa mkisubiri kuipeleka machinjioni kuhakikisha mnaitoa na kuitafutia eneo jingine kwa ajili ya kuitunza,” alisema Naibu Waziri Gekul.
Aidha, Naibu Waziri Gekul aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa wizara imeshatenga fedha zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuanza kuboresha miundombinu ya mnada huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ukuta unaozunguka mnada huo.
Vilevile ametoa rai kwa wananchi kutovamia eneo la mnada, kwani moja ya sababu iliyochelewesha kuanza kwa ujenzi wa ukuta huo ni migogoro iliyotokana na uvamizi wa ardhi. Pia amewataka viongozi katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kuhakikisha wanasimamia na kuchukua hatua mapema pale wanapoona mtu anavamia maeneo haya ya minada.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema kuwa timu ya wataalam inayofanya uhakiki wa eneo hilo kutokana na uvamizi itakapomaliza kazi yake watahakikisha wanalipima eneo hilo kwa haraka
Post A Comment: