Na Asteria Muhozya, Dodoma
Imeelezwa kuwa, kufuatia kukamilika kwa Ujenzi wa Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani Mwaka 2018 , udhibiti wa madini hayo umeimarika na hivyo kupelekea kuongezeka kwa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali kutoka shilingi milioni 238 Mwaka 2016 na 2017 hadi kufikia shilingi bilioni 1.417 Mwaka 2020.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakati akiwasilisha taarifa ya Eneo Tengefu la Mirerani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika kikao kilichofanyika Machi 10, jijini Dodoma.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, ukuta huo umewezesha kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini yaliyokuwa yakiisababishia Serikali hasara , kuimarisha ulinzi wa watu wanaofanya shughuli mbalimbali na mali zao ndani ya ukuta ikiwemo kurahisisha shughuli za kiutawala na usimamizi wa rasilimali madini katika eneo hilo na kuzuia utumikishwaji wa watoto katika shughuli za uchimbaji madini ya tanzanite.
Aidha, Prof. Msanjila ameieleza kamati hiyo kuwa, Kituo cha Pamoja cha Biashara ya Tanzanite (One Stop Center) kilichojengwa ndani ya ukuta huo, sasa ni rasmi kuwa, kitajulikana kwa jina la Kituo cha Tanzanite cha Magufuli, (Magufuli Tanzanite Center).
Ameongeza kuwa, kituo hicho ambacho tayari kinafanya kazi, kinahusisha ofisi mbalimbali zikiwemo za Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Jeshi la Polisi, Ukumbi wa Mikutano na Ofisi ya Madini.
Amezitaja ofisi nyingine katika kituo hicho kuwa ni pamoja na Vyumba vya Mahabusu, Chumba cha Uthaminishaji Madini, Mabenki, Chumba cha Usimamizi wa CCTV Kamera, Chumba maalum cha kuhifadhia madini na server room.
Aidha, Prof. Msanjila ameileza kamati hiyo kuhusu miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika eneo hilo la Mirerani ikiwemo ile inayoendelea kutekelezwa ambapo ameitaja kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya ndani inayozunguka ukuta, mradi wa ujenzi wa Vyumba viwili vya upekuzi , eneo la kupumzika wadau wa madini na soko la madini.
Katika hatua nyingine, akizungumzia manufaa ya kituo cha Kituo cha mfano kwa wachimbaji wadogo cha Katente kilichopo mkoani Geita, Prof. Msanjila amesema kimewezesha kuzalishwa kwa kiasi cha gramu 11. 588.37 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo 39.
Ameongeza kuwa, uwepo wa kituo hicho umewezesha kufanyika kwa malipo ya shilingi 104,038,097.73 za mrabaha na ada za ukaguzi wa madini na tozo za Halmashauri kwa Wilaya ya Bukombe na Geita na upatikanaji shilingi 72,551,065.53 kutokana na huduma zilizotolewa kwa wachimbaji wadogo .
Vituo vya mfano vilianzishwa na serikali kupitia wizara ya madini kwa lengo la kutoa huduma za uchimbaji na uchenjuaji madini kama vile usagaji mawe, ukamatishaji wa dhahabu kwa kutumia sayanadi, ukamati dhahabu kwa kutumia mitambo ya elusion na ukodishaji wa vifaa vya uchimbaji. Huduma hizo zinalenga kutolewa kwa kutumia miundombinu iliyoanzishwa kwa kutumia teknolojia nafuu na rahisi kuigwa ambazo zina mchango katika uendelezaji wa uchimbaji mdogo nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba akiwasilisha taarifa ya Soko Kuu la dhahabu Geita, ameieleza kamati hiyo kuwa, madini yanayozalishwa na kuuzwa katika Soko la Geita yamekuwa yakiongezeka toka soko lilipoanzishwa mwezi Machi 2019, kutoka wastani wa kilogramu 160 za dhahabu kwa mwezi hadi kilogram 450 za dhahabu kwa mwezi.
Ameongeza kuwa, kabla ya mfumo wa masoko ambao kwa kiasi kikubwa umeimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali, kiwango cha uzalishaji kilikuwa kilogramu 124.3 mwezi Novemba na kiwango cha chini kilogramu 61.3 mwezi Oktoba.
‘’Baada ya mfumo wa masoko kuanzishwa, kiwango cha juu cha uzalishaji wa dhahabu kimeripotiwa kuwa kilogramu 537.6 kwa mwezi Oktoba 2019, na chini ikiwa ni kilogramu 167.7 mwezi Aprili, 2019’’ amesema Samamba.
Katika kikao hicho, Kamati ya Bunge imeishauri wizara kuendelea kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti utoroshaji wa madini na mikakati itakayowawezesha wachimbaji wadogo kuzalisha zaidi madini hivyo kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Baada ya uwasilishaji wa taarifa hizo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini inatarajia kutembelea miradi kadhaa inayotekelezwa na wizara na Taasisi zake.
Post A Comment: