Na Atley Kuni, Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Selemani Jafo, ameagiza ifikapo Julai 30, 2021, mradi wa ujenzi wa barabara katika mji wa Serikali eneo la Mtumba uwe umekamilika. Agizo la Waziri Jafo linafuatia taarifa iliyosomwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Barabara za Mijini na Vijijini kutoka TARURA Mhandisi Mohammed Mkwata kuwa ujenzi wa barabara hizo upo nyuma kwa asilimia 6 kutokana na kukosekana kwa saruji yenye mgandamizo mwepesi yenye ujazo wa 32.5N na badala yake saruji inayopatikana kwa wingi ni ile yenye mgandamizo wa juu aina ya 42.5N.


Mhandisi Mkwata ameeleza kuwa ujenzi ulitarajiwa kufikia asilimia 69 badala ya 63 za sasa kulingana na mpango kazi wa mkandarasi kutokana na uhaba wa saruji katika kipindi cha kuanzia Novemba 26 mwaka 2020 hadi mwishoni mwa februari 2021. 


“Katika kipindi hicho mkandarasi hakuweza kupata saruji aina zote za 32.5N na 42.5N kwa kadiri ya mahitaji halisi hali ambayo iliathiri kazi za ujenzi wa vivuko na ujenzi wa tabaka la kwanza la barabara ambalo nalo linahitaji saruji,” amesema.


 Kufuatia taarifa hiyo Waziri Jafo ameitaka TARURA kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara hizo za mji wa serikali kwa kiwango cha lami unakamilika Julai 30, mwaka huu na kuwa kama kikwazo ni kukosekana kwa saruji hiyo nyepesi basi waangalie uwezekano wa kutumia saruji yenye mgandamizo wa juu. 


“Sijaridhishwa na kasi hii maana ipo chini kwa asilimia sita kwa maana hiyo sihitaji mjadala wa aina yoyote nataka ifikapo Julai 30 mradi huu uwe umekamilika, haiwezekani uchelewe kwa kigezo cha kukosekana Saruji aina ya 32.5N hivyo angalieni namna ya kutafuta suluhisho ya hili,” amesema Jafo.


 Waziri Jafo amewataka Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA waifanyie utafiti wa kimaabara saruji aina ya 42.5N ambayo kwa sasa inapatikana madukani ili kuona kama inafaa kutumika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara hizo katika mji wa serikali. 


Katika hatua nyingine, Waziri Jafo ametembelea mradi wa barabara ya kuingia Hospitali ya Uhuru iliyopo Halmashauri ya wilaya Chamwino inayotakiwa kukamilika ifikapo Machi 14, 2021, ambapo ameelezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kuahidi kuwa ifikapo Machi 15 atafika eneo hilo tena kuona ujenzi ulivyokamilika.


 Awali, akitoa taarifa za mradi, Meneja wa TARURA kutoka halmashauri ya wilaya ya Chamwino, Mhandisi Nelson Maganga alisema kuwa, maendeleo ya jumla ya utekelezaji wa mradi yamefikia asilimia 85. 


Waziri Jafo, amefanya ziara katika miradi hiyo miwili, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara anazozifanya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kutolea maelekezo kwa watendaji wa serikali.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: