TUMUUNGE Mkono Mama! Ni kauli ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umeahidi kumpa ushirikiano wa bega kwa bega Rais Samia Hassan Suluhu huku ukimpongeza kwa kuteuliwa kwake Katika nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba .
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 28,2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Kheri James,wakati akizungumza na waandishi wa habari,amesema kuwa UVCCM ina imani kubwa na Rais Mama Samia kwa miaka takribani miaka mitano aliyohudumu kama Makamu wa Rais alionesha upendo wake na ushirikiano mkubwa kwa vijana.
Amewatoa hofu vijana na watanzania kuwa licha ya kumpoteza kiongozi shupavu, Dk John Magufuli ambaye alifariki Machi 17 mwaka huu lakini uwezo alionao Mama Samia ni mkubwa na anatosha kuvaa viatu vya Dk Magufuli katika kuwatumikia watanzania.
“Tuna Imani na Mama Samia kwa kuwa tumefanya nae kazi na tunatambua kuwa yeye ni mlezi kwa vijana hivyo niwatoe wasiwasi vijana nchini ambao wanawaza Dkt Magufuli hayupo hali itakuwaje ,huyu Mama ataendelea kuwa mtetezi wetu,”amesema Kheri James.
Kheri amesema katika hotuba ya Mama Samia wakati anaapishwa alisema huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kudumisha mshikamano na siyo wakati wa kunyoosheana vidole hivyo kuwataka watanzania wote kuiunga mkono kwa kushikamana na kufanya kazi.
” Jukumu letu la msingi kama vijana ni kuhakikisha tunaisimamia dhamira aliyonayo Rais wetu Mama Samia ya umoja na mshikamano na sisi tuna wajibu wa kumuunga mkono, tusiwe sehemu ya chuki na kama huko nyuma kuna mahali tulikwazana tunaomba radhi lengo liwe kutengeneza jukwaa safi la Rais wetu katika kuwatumikia watanzania.
Niwasisitize vijana wa CCM na vyama vingine kumrahisishia kazi Rais wetu ya kusonga mbele, tunaweza kutofautiana kwenye itikadi lakini linapokuja suala la umoja tushikamane na kuitumikia wote nchi yetu,” Amesema Kheri James.
Amewatoa hofu vijana kuwa yale yote yaliyoahidiwa kwenye kampeni na Dk Magufuli yataendelea kutekekezwa na Rais Mama Samia na yeye kama muwakilishi wa vijana ataendelea kusimamia na kukumbusha ahadi zote zinazowahusu vijana ili ziweze kutimizwa.
” Ni kweli tumempoteza kiongozi wetu Dk Magufuli niwatoe hofu kilichokufa ni kiwiliwili chake tu ila fikra na misingi ya kazi aliyoitengeneza itaendelea kudumu kwa miaka mingi zaidi, tuna imani kubwa kama vijana na uongozi wa Mama Samia tuliona uwezo na kasi yake akiwa Makamu hatuna shaka nae na sisi kama vijana tunamuahidi tupo nae bega kwa bega,” Amesema Kheri James.
Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa ametoa pongezi kwa Abdul Nondo ambaye kwa kipindi kirefu ameonyesha kuwa kinyume na mambo yanayofanywa na Serikali lakini kwa kipindi hiki yupo bega kwa bega katika kuwahamasisha vijana wengine kumuenzi Hayati Magufuli.
Katika hatua nyingine ameeleza kuwa uongozi wa UVVCM unatarajia kukutana kujadili namna bora ya kumuenzi Hayati Magufuli kutokana na mengi aliyoyafanya kwa watanzania.
Post A Comment: