Na Dotto Mwaibale, Morogoro
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) inatarajia kuanza kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuwanufaisha watanzania.
Hayo yalielezwa katika Kikao cha Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi wa TIA lililoketi Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ( SUA) mkoani Morogoro ambacho kilikuwa na ajenda 11.
Kabla ya kuanza kikao hicho wajumbe wote wakiongozwa na Mwenyekiti wao Profesa Carolyne Nombo walisimama kwa dakika moja ikiwa ni ishara ya kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt.John Pombe Magufuli.
Akizungumza katika kikao hicho Profesa Carolyne Nombo alisema mafunzo hayo yataanza kutolewa hivi karibuni.
"Tupo kwenye mchakato wa kuanza kutoa mafunzo haya na tukisha kamilisha kufanya utafiti tutaanza kuyatoa mapema iwezekanavyo." alisema Nombo.
Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma Dkt. Momole Kasambala akizungumzia ajenda nyingine alisema chuo hicho kitaanzisha mahusiano na ushirikiano na vyuo vya ndani na nje ili kubadilishana uzoezi wa ufundishaji na mambo mengine na tayari wapo katika hatua ya kuandaa maridhiano ya pamoja baina yao na Chuo Kikuu cha Irkutsk cha Urusi ili kuanza rasmi kushirikiana katika nyanja kadhaa zitakazoainishwa kwenye mkataba huo.
Alisema katika maazimio ya kikao cha baraza hilo la mwaka jana waliazimia kuingia mikataba na benki za Posta, CRDB na NMB lengo likiwa ni kuongeza wigo wa mikopo yenye riba nafuu kwa wafanyakazi ambapo tayari wamekwisha fanya mkataba na Benki ya NMB kwa riba ya asilimia 15.
Post A Comment: