Na Dotto Mwaibale, Singida
WANAWAKE wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wameanza kupata afueni ya kiuchumi baada ya kupatiwa mafunzo ya kilimo cha mboga mboga na matunda na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a alisema wametoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa ni kuwakomboa wanawake hao kiuchumi.
Alisema TAHA inaendesha kazi zake katika mikoa 23 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja ( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba
( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) na kuwa sasa wameongeza wilaya mbili moja, Ikungi-Singida na Msalala-Shinyanga na kufikisha mikoa 25 ambayo wanatekeleza mradi huo.
Alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi.
Shang'a aliwataja wadau wanao wawezesha katika mnyororo huo wa thamani kuwa ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.
" Katika uwezeshaji wetu kazi kubwa tunazozifanya naweza nikasema ni tatu lakini nitaongeza ya nne ya kwanza ikiwa ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo." alisema Shang'a.
Alitaja kazi ya tatu kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.
Shang'a alitaja kazi ya nne na ya mwisho kuwa ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliipongeza Asasi hiyo ya TAHA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN WOMEN) kwa kutoa mafunzo hayo na akaahidi kushirikiana na asasi hiyo na wadau wote.
Kwa upande wake Mariam Rashid akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake waliopata mafunzo hayo alisema yanaenda kuwapunguzia mzigo katika familia zao kwani yatawasaidia kuwainua kiuchumi na kuacha kuwategemea wanaume wao kwa kila kitu.
Post A Comment: