Na.Catherine Sungura,Dar es Salaam
Serikali imepongezwa kwa kutenga shilingi bilioni 15.5 kwa ajili ya uwekezaji wa Mradi wa Ujenzi wa kituo cha Kisasa cha kufanya Vipimo vya Saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia (PET CT Scan) pamoja na kiwanda cha kuzalisha Mionzi dawa (Radio Isotopes).
Pongezi hizo zimetolewa leo na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo, wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), iliyopo Dar es Salaam.
Mhe.Nyongo amesema kuwa Serikali imeipa kipaumbele sekta ya afya, uwekezaji wa mradi huo utakuwa ni wa kihistoria, wa kimkakati na kwamba utaiweka Tanzania kwenye dira ya kimataifa kwenye eneo la afya.
Amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia watanzania na hata wageni kutoka nje ya nchi kupata matibabu sahihi na kwa wakati ya saratani.
“Hatua hii ni kubwa, mradi huu itasaidia watu wengi kupata huduma hizi za kibingwa kwa wakati kwani watu wengi walikuwa wanafika kupata huduma wakiwa Kwenye hatua za mwisho,” amesema.
Ameongeza kwa kiwanda hiki wananchi wengi watajua hali zao mapema na uchunguzi utaonesha ugonjwa umeenea kiasi gani mwilini na Taasisi itakwenda kutambulika mapema zaidi na kuwatibu na hii ikiwa ni pamoja na magonjwa mengine.
“Ni hatua kubwa watu wengi watakuja Tanzania kufuata huduma ya vipimo, na Watanzania watanufaika, watapata tiba sahihi na kwa wakati sahihi, ni jambo kubwa Sana, mnastahili kupongezwa.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mionzi dawa, alisema ni maamuzi sahihi yaliyofanyika kwa wakati sahihi.
“Mmepitia michakato yote, kamati inawapongeza sana, uwekezaji huu unakwenda kufungua mipaka ya uwekezaji kwa sekta binafsi vile vile, kwamba mwekezaji yoyote kwa mfano kutoka India na kwengineko anaweza kuwekeza Tanzania kwa sababu tuna kiwanda hapa,” alisema.
Alisema uwekezaji huo itakwenda kuongeza fursa ya utalii wa kimatibabu (medical tourism) kwa Tanzania kwani watu wengi watapenda kuitembelea.
Kwa upande wa bima ya afya kwa wote Mhe.Nyongo amesema hatua hiyo ni nzuri kwani itasaidia wananchi wengi kwakuwa huduma za saratani ni gharama kubwa.
“Niwapongeze Ocean Road kwa kuendelea kutoa matibabu bure lakini lazima suala la bima kwa wote tukienda nalo, litamaliza tatizo la changamoto ya gharama kubwa za matibabu, tutapenda (Wizara) mtuletee mpango huu, tupo tayari tuhakikishe tupo bega kwa bega, tulichakate pamoja na tulifikishe bungeni, tuweze kuipitisha,” amesisitiza.
Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani ni tatizo kubwa duniani na matibabu yake ni ghali Sana.
Amesema Serikali inafanya Mapinduzi katika kukabiliana na Magonjwa hayo kwani yanachukua watu wengi(kifo) hata hivyo yanazuilika, ni muhimu jamii kujua namna gani ya kukabiliana nayo ikiwemo kufanya mazoezi.
“Serikali ni makini hivyo tunapoelekea Kwenye Bima ya afya kwa wote itasaidia, hata hivyo wizara inatoa msamaha kwa wagonjwa wote wasio na uwezo ambapo hufuata taratibu zote za msamaha.
Dkt.Gwajima alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata uchunguzi wa Afya zao ili waweze kupata matibabu mapema.
Post A Comment: