Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi,akizungumza katika kikao hicho cha tathmini.
Na Peter Kashindye, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amepokea vifaa tiba na chakula dawa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 100 vilivyotolewa na Shirika la Action Against Hunger la mjini hapa.
Akipokea vifaa hivyo katika kikao cha tathimin ya mkataba wa lishe, tamko la jiongeze tuwavushe salama na CHF iliyoboreshwa kilichofanyika jijini hapa leo, Dkt. Nchimbi amewataka waganga wakuu wa wilaya na halmashauri mkoani hapa kutumia vifaa hivyo kwa walengwa ili kuimarisha afya za wananchi.
Dkt. Nchimbi alisema thamani halisi ya vifaa hivyo pamoja na dawa inaonekana kwa kuangalia wananchi ambao wanaenda kuhudumiwa.
“Mama huyu atakayehudumiwa ni mama ambaye anawajibu na utumishi kwa familia pana na kwa kila mmoja atakaye hudumiwa atakuwa anawakilisha familiya au kaya ya watu nane au kumi na hapo atakuwa amehudumia mkoa na taifa kwa ujumla”. alisema.
Dkt. Nchimbi, aliwataka maafisa hao wa afya waliopokea vifaa hivyo kuwa waaminifu na kumtanguliza Mungu.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Ibrahim Pazia amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambao utatumika kwa ajili ya wananchi wa wilaya hiyo ambapo ameahidi kuvitunza na kuvitumia kwa manufaa ya wananchi na si vinginevyo.
“Tumepokea vifaa tiba zaidi ya vitanda 21 vyenye magoro yake pamoja na mashuka, vifaa vya upumuaji na vifaa vingine vya kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kuwa vimefika wakati muafaka.” Alisema.
Kwa upande wake Meneja Mratibu wa Shirika hilo, Daudi Tano alisema shirika hilo limetoa msaada huo ikiwa ni kuendelea kuunga jitihada za Serikali katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za lishe katika mkoa na halmashauri.
Alisema kupitia mradi huo wa lishe imara wameweza kusaidia vifaa hivyo na chakula dawa ambavyo ni muhimu sana kwa watoto wenye utapiamlo katika halmashauri za wilaya za Itigi, Iramba na Mkalama.
Alisema vifaa walivyokabidhi ni pamoja na boksi 400 za chakula dawa ambazo zitawafikia watoto wengi. Pia shirika limejenga kituo kimoja cha matibabu ya utapiamlo katika halmashauri ya Iramba ambacho kitahudumia halmashauri hiyo na jirani.
Post A Comment: