MBUNGE
wa Kisesa, Luhaga Mpina akihojiwa na waandishi wa habari wakati akiwa msibani Chato |
MBUNGE
wa Kisesa, Luhaga Mpina amemlilia aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John
Pombe Magufuli akimtaja kama kiongozi wa mfano na kielelezo barani
Afrika katika kuleta maendeleo na kushughulikia kero na matatizo ya
wananchi yaliyoshindikana kwa miaka mingi.
Mpina
ambaye katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Magufuli aliwahi kuwa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na baadae
kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Akizungumza
mara baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Dk.
Magufuli kwenye uwanja wa Magufuli mjini Chato, Mpina alisema taifa
limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kiongozi makini na shujaa ambaye
alitumia muda wake wote wa uongozi kusaka maendeleo ya nchi huku
akikomesha na kumaliza dhuluma na vikwazo vilivyokuwepo dhidi ya ustawi
wa jamii, uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
“Nilizipokea
taarifa za kifo cha Mhe. Rais Dk. Magufuli kwa huzuni na majonzi
makubwa nililia kwa kupaza sauti zaidi ya saa moja na baadae machozi
yaliendelea kutiririka kama maji nikiwa sijui hata la kufanya jitihada
za kuninyamazisha na kufuta machozi hazikuwezekana, tangazo la kifo cha
kiongozi huyu ilikuwa ni mkuki uliochoma moyo wangu na kuujeruhi sana,
Kiongozi nimpendaye mchakapazi na hodari asiyeyumba wala kuyumbishwa
katika maamuzi asiyechoka kupambania taifa lake na asiye na rekodi ya
kushindwa jambo lolote kweli ndio hatunaye tena” alisema Mpina.
Mpina
amesema maamuzi ya mwenyezi Mungu hayana rufaa na hayahojiwi popote
tumebaki wakiwa na majonzi yasiyokufani Mungu atabaki kuwa Mungu na
mwenye mamlaka yote, hivyo tunamuomba Mungu wa mbinguni amuongoze Rais
wetu Samia Suluhu Hassan katika kuliongoza taifa letu kwa bidii na
upendo mkubwa.
“Nimehudumu
kama Naibu Waziri kwenye iliyokuwa ofisi yake ya Makamu wa Rais hivyo
Sina mashaka kabisa na utashi, uwezo, dhamira na kipaji cha wa Mhe.
Rais Samia katika kuhakikisha kuwa taifa linasonga mbele kwa mafanikio
makubwa namuomba Mungu azidi kumwagia Baraka ili ndoto za mafanikio ya
taifa letu zifikiwe” alisema Mpina.
Alisema
Rais Magufuli kwa muda mfupi wa miaka mitano alipambana na kufanikiwa
kukosemesha vita dhidi ya madawa ya kulevya ambapo sehemu kubwa ya
vijana waliangamia alidhibiti na kuvunja mitandao ya biashara hiyo
haramu hapa nchini ambapo madawa yaliyoingizwa nchini yalikamatwa na
kutaifishwa na Serikali na jumla ya watuhumiwa 37,104 walitiwa mbaroni
ambapo imepelekea kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya nchini kwa
asilimia 90.
Kuhusu
Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, Mpina amesema Rais Magufuli
alikuwa kiongozi wa kwanza kuanzisha Mahakama ya Uhujumu Uchumi ambapo
watu wote bila kujali nafasi zao wamefikishwa kwenye mahakama hiyo pia
aliipa meno TAKUKURU kushughulika na wala rushwa ambapo kwa miaka
mitano rushwa imepungua kwa kiasi kikubwa nchini, Serikali yake
imefanikiwa kurejesha mali za umma zilizochukuliwa na watu binafsi ama
taasisi kinyume cha sheria na pia ameweza kuokoa kiasi cha shilingi
bilioni 273 zilizokuwa zimeibiwa.
Pia
Rais Magufuli alifanikiwa kukomesha ujangili na ujambazi ambapo kabla
ya hatua zake biashara ya pembe za ndovu na nyara zingine za Serikali
ilipamba moto katika taifa letu na wanyama wengi kuuawa na kusafirishwa
hai kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria, majambazi yalitamba kila kona
na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Hatua alizochukua Rais
Magufuli zimemaliza vitendo hivyo na mapato yatokanayo na utalii
yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi Dola za
Marekani bilioni 2.6.
Mpina
alibanisha kuwa kabla ya Rais Magufuli mauaji ya vikongwe na albino
yalikithiri kila kona ya nchi na kufanya kundi la wananchi hao kuishi
kwa hofu na fedheha kubwa ndani ya nchi yao ambapo kwa muda mfupi wa
uongozi wake vitendo hivyo vimekomeshwa na sasa makundi haya yanaishi
kwa amani na kushiriki shughuli za kiuchumi bila wasiwasi wowote .
Pia
Mpina kabla ya Rais Magufuli uvuvi haramu ulitamalaki kila kona
kunakofanyika shughuli za uvuvi na kusababisha samaki kupungua kwa kiasi
kikubwa hali iliyochangia viwanda vingi vya samaki kufungwa huku mauzo
ya samaki nje ya nchi yakiporomoka na nchi kutegemea samaki wa kutoka
nje ya nchi, kwa upande wa pwani uvuvi haramu wa kutumia mabomu
ulisababisha watu wengi kupoteza maisha na kupata ulemavu wa kudumu wa
viungo.
Kutokana na hali
hiyo Rais Magufuli alichukua hatua thabiti ya kudhiti uvuvi haramu
nchini ambapo uvuvi wa kutumia mabomu umedhibitiwa kwa asilimia 100 na
uvuvi wa kutumia zana haramu umedhibitiwa kwa asilimia 80 hali
iliyopelekea ongezeko kubwa la samaki, viwanda kuongezeka, kupungua kwa
uagizaji wa samaki kutoka nje ya nchi kutoka thamani ya tsh. Bilioni 56
kwa mwaka hadi tsh. bilioni 0.16 kwa mwaka, mauzo ya samaki nje ya nchi
yameongezeka kutoka bilioni 379 mwaka 2015 hadi bilioni 692 mwaka 2019
hayo ni mafanikio makubwa ya Dk. Magufuli.
Kuhusu
kuongeza ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa upotevu wa mapato ya
Serikali, alisema Rais Magufuli aliweka mifumo imara ya TEHAMA, alipanua
wigo wa walipa kodi, kupunguza misamaha ya kodi, kufuta mikataba ya
kinyonyaji, kudhibiti utoroshaji wa fedha na rasilimali nyingine kwenda
nje ya nchi.
Kutokana na
jitihada hizo Mpina alisema ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa mwezi
umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi
wastani wa shilingi trilioni 2 kwa mwezi mwaka 2020. Kwa ujumla mapato
ya ndani yameongezeka kutoka trilioni 11 mwaka 2015 hadi kufikia
trilioni 18.5 mwaka 2019.
Pia
Mpina alisema wakati Dk John Magufuli anaingia madarakani nchi yetu
ilikuwa miongoni mwa nchi zinazotorosha fedha nyingi za umma kwenda nje
ya nchi kinyume cha sheria na bila kulipa kodi stahiki za Serikali
(Illicit Financial Flows).
Mpina
aliongeza kuwa makampuni ya kimaitaifa yaliyowekeza na kufanya biashara
nchini hususani makampuni ya simu, madini na gesi yalikuwa yakiongeza
gharama za uwekezaji kwa lengo la kukwepa kodi (Transfer Pricing) na
kuisababishia Serikali kukosa mapato.
Dk.
Magufuli alichukua hatua mahususi ya kumaliza tatizo sugu la utoroshaji
wa fedha na uongezaji gharama ambapo tulishuhudia kufutiwa kwa leseni
baadhi ya mabenki na maduka ya kubadilisha fedha yaliyokiuka sheria za
usimamizi wa fedha. Pia mifumo thabiti ikawekwa ya usimamizi na matumizi
ya fedha za kigeni nchini pamoja na kutungwa sheria mpya kuongeza
udhibiti.
Mpina alisema
mbali na hayo pia Rais Magufuli alifuta mikataba ya kidhalimu iliyokuwa
ikilinyonya taifa kila uchao ambapo alizima mitambo ya IPTL, Aggreko na
Syimbion na kuokoa shilingi bilioni 719 kwa mwaka.
Mpina
alisema Rais Magufuli alidhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma kwa
kuzuia au kupunguza safari za nje zisizo za lazima, semina, warsha,
makongamano, matamasha na udanganyifu kwenye manunuzi.
Kutokana
na jitihada kubwa alizofanya Dk. Magufuli katika udhibiti na usimamizi
wa mapato na matumizi umewezesha nchi yetu kuongeza bajeti ya maendeleo
kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40 na ndio chimbuko kwa nchi
kuanza kujenga miradi mikubwa kwa fedha za ndani ikiwemo Reli ya SGR na
Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.
Alisema
Dk. Magufuli alianzisha mfumo wa utoaji elimu bila malipo kwa shule za
msingi na sekondari ambapo umetoa unafuu mkubwa kwa watoto masikini
kuweza kupata haki ya elimu hali hiyo imewezesha ongezeko la vijana
wengi kusajiliwa kujiunga na masomo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Aidha
Rais Magufuli aliendelea kuishangaza nchi alipokuwa akiongeza bajeti ya
mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka 2014/2015
hadi shilingi bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020 na kuwezesha
vijana wengi kupata mikopo na kuendelea na masomo ya juu.
Kwa
upande wa sekta ya afya, Mpina alisema kwa kipindi kifupi cha uongozi
wa Dk. Magufuli vituo vipya vya kutolea huduma za afya 1,769 vimejengwa
huku bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka shilingi
bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 270 hivi sasa
Pia
Rais Magufuli aliimarisha matibabu ya kibingwa nchini hususan magonjwa
ya moyo, mifupa na figo ambapo imewezesha idadi ya rufaa za kwenda nje
ya nchi kupungua kwa asilimia 95 ambazo zilikuwa zikiingarimu nchi fedha
nyingi huku wagonjwa wasio na uwezo wa kwenda nje ya nchi walikufa
bila matibabu.
Mpina
alisema Rais Magufuli aliimarisha huduma za mawasiliano kwa kuongeza
usikivu wa simu kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 94 mwaka
2020 na kuwezesha kupungua kwa gharama za kupiga simu kwa dakika moja
kutoka shilingi 267 mwaka 2015 hadi shilingi 40 tu hivi sasa hali
iliyoleta unafuu mkubwa kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia sekta
hiyo.
Mpina alisema Rais
Magufuli amesimamia ujenzi wa barabara na madaraja mengi nchi nzima
akiwa Waziri wa Ujenzi na baada ya kushika wadhifa wa urais kwa kipindi
cha miaka mitano amewezesha kujengwa na kukamilika barabara za lami
zenye jumla ya kilometa 3,500 pia Barabara nyingine zenye urefu wa
zaidi ya kilometa 2,000 zinaendelea kujengwa kote nchini na kurahisha
shughuli za kiuchumi na kijamii.
Pia
Rais Magufuli amejenga madaraja makubwa 13 yaliyoshindikana kujengwa
kwa miaka mingi na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
amejenga barabara za juu (flyover na interchange) Dar es Salaam za
Kijazi na Mfugale pamoja na barabara ya njia nane kutoka Kimara kwenda
Kibaha ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar
es Salaam.
Rais Magufuli
aliamua kujenga reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza
ambapo utekelezaji wake uko kwenye hatua mbalimbali mradi huu mkubwa
unajengwa kwa fedha za ndani. Pia usafiri wa reli ya Dar es Salaam
–Tanga – Moshi - Arusha, ambao ulisimama kwa takriban miaka 20. Lakini,
katika kipindi chake alifanikiwa kurudisha tena usafiri wa treni kutoka
Dar es Salaam kwenda Tanga, Moshi hadi Arusha na kurahisha shughuli za
usafiri na uchukuzi.
Aliongeza
kuwa bandari nyingi zimepanuliwa katika ukanda wa Pwani na maziwa ya
Victoria, Tanganyika na Nyasa pamoja na kujenga na kukarabati meli
zilizokuwa zimetelekezwa kwa miaka mingi ambapo Ziwa Victoria pekee
amekarabati meli tano na kujenga Chelezo moja kubwa kwa ajili kujenga
na kukarabati meli hizo.
Mpina
alisema Rais Magufuli amejenga wa viwanja vya ndege vipya 11 na kununua
ndege mpya 11 za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kupelekea
kuongezeka kwa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.
Mpina
aliongeza kuwa Dk. Magufuli alifanya maamuzi yaliyoshindikana kwa miaka
mingi na kuanza ujenzi wa Mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere kwenye
Bonde la Mto Rufiji. Mradi huu unagharimu shilingi trilioni 6.5 na
utakapokamilika utazalisha umeme Megawati 2115 ambapo itapunguza gharama
za umeme na kumaliza tatizo la upungufu wa umeme nchini.
Pia
Mpina alisema kupitia Mradi wa REA Dk. Magufuli katika kipindi chake
kifupi ameongeza idadi ya vijiji vilivyofikishiwa umeme kutoka 2,018
mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwezi Aprili 2020 na jumla ya viwanda vipya
8,477 vimejegwa nchini na kupunguza tatizo la ajira.
Mpina
alisema kabla ya Dk. Magufuli hajaingia madarakani wafugaji walifukuzwa
kama wakimbizi kwenye nchi yao na kutakiwa kurudi walikotoka, migogoro
ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ilishamiri na kusababisha
mapigano yasiyokoma ambapo walijeruhi na kuuana pia mifugo mingi
ilikufa kwa kukatwa mapanga na kuwekewa sumu na mingine kutaifishwa.
Mpina
alisema Hayati Dk. Magufuli alipunguza kwa kiwango kikubwa migogoro
hiyo kwa Serikali yake kufanya ziara maeneo yenye migogoro na kuunda
timu ya mawaziri nane, alichukua uamuzi wa kurasimisha vijiji 920
vilivyoanzishwa ndani ya hifadhi.
Pia
alisema Dk. Magufuli alifuta baadhi ya hifadhi na mashamba ya Serikali
na kugawa ardhi hiyo kwa wananchi ili itumike kwa shughuli za kilimo na
ufugaji pia katika kukabiliana na magonjwa ya mifugo nchini alijenga
majosho mapya 104 na kukarabati majosho 542 yaliyokuwa yametelekezwa kwa
zaidi ya miaka 30 na ameimarisha utoaji chanjo za mifugo na kuanzisha
kampeni ya uogeshaji mifugo kwa dawa za ruzuku kote nchini, Pia
ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mifugo na uvuvi yaliongezeka kutoka
wastani tsh bilioni 21 mwaka 2015 hadi kufikia tsh bilioni 74 mwaka
2020.
Mpina amesema
katika kipindi chake Rais Magufuli aliweza kutatua tatizo la ukosefu wa
mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ambapo Serikali imeipa TADB
shilingi bilioni 325 ili kuongeza uwezo wa kutoa mikopo kwa wakulima,
wafugaji na wavuvi nchini ambao kwa miaka mingi walikuwa hawakopesheki.
Mpina
alibainisha kuwa katika kipindi cha Magufuli alifanikiwa kumaliza
tatizo la uvuvi haramu ambapo tulishuhudia wingi wa samaki pamoja na
Samaki wakubwa kupatikana mfano sangara kwenye Ziwa Victoria
waliongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka
2020, na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16
hadi sentimeta 25.2.
pia
Uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika vitotoleshi vya Serikali na
Sekta binafsi uliongezeka kutoka 8,090,000 mwaka 2015 hadi kufikia
vifaranga zaidi ya 50,000,000 mwaka 2020. Kutokana na uzalishaji huo
hivi sasa nchi yetu haiagizi vifaranga vya samaki tena kutoka nje ya
nchi.
Mpina alisema
katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli sheria nyingi mpya
zilitungwa na zingine kufanyiwa marekebisho ili kulinufaisha taifa
akitolea mfano wa Sheria ya kulinda rasilimali za taifa( The Natural
Weath and Resources -Permanent Sovereignty –Act 2017) sheria hii
imewezesha kuanzishwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Company ambapo
Serikali yetu inamiliki hisa asilimia 16 na Kampuni ya Barrick asilimia
84 ya Hisa utaratibu huu haukuwepo hali iliyosababisha nchi kutopata
mapato stahiki katika madini na gesi.
Mpina
aliongeza kuwa kutokana na hatua alizochukua Rais Magufuli mapato
yatokanayo na madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 194 mwaka
2016 hadi wastani wa shilingi bilioni 500 mwaka 2020.
Pia
Rais Magufuli alikomesha dhuluma kwa wachimbaji wadogo ambapo kila
walipokuwa wanagundua madini walifukuzwa kama wakimbizi ndani ya nchi
yao ili kupisha wawekezaji lakini chini ya utawala wake wametengewa
maeneo na wanafanya kazi ya uchimbaji vizuri na kujipatia kipato.
Hata
hivyo Mpina alisema kutokana na jitihada zake hizi Rais Magufuli
aliiwezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi
na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi Barani
Afrika.
“Nikupe zawadi
gani Dk. Magufuli kwa wema uliolitendea taifa lako katika kipindi
kigumu na chenye vitisho vingi hukusita kuchukua maamuzi, hukukubali
kutishwa, kuyumbishwa wala kukatishwa tamaa na mtu yoyote au taasisi za
kimataifa katika kufanya maamuzi sahihi kwa taifa lako ambapo uimara
wako huo ndio umepelekea nchi yetu kupiga hatua kubwa za kimaendeleo na
kiuchumi ambapo kumepelekea nchi yetu kuingia uchumi wa kati ndani ya
miaka mitano badala ya miaka 10 iliyotarajiwa” alisema Mpina
Mpina
alisema pia Rais Magufuli alikuwa mtetezi wa wanyonge ambapo katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita aliyakumbuka makundi ambayo yalikuwa
hayathaminiwi na kufanyiwa kila aina ya dhuluma na baadhi ya watendaji
wa Serikali kama Mama ntilie, Bodaboda na Machinga ambapo dhuluma
zilikomeshwa kwa kutengewa maeneo biashara na kuondolewa mzigo mkubwa wa
ushuru uliokuwa unawaelemea kila uchao kwa kutengenezewa vitambulisho
vya wajasiriamali.
Pia
Rais Magufuli alifanikisha kutungwa Sheria yenye kuzitaka halmashauri
zote kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo
na riba kwa wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na wenye ulemavu
(asilimia 2), ambapo hadi mwezi Machi 2020 kiasi cha shilingi bilioni
93.2 kilikuwa kimetolewa.
“Dk.
John Pombe Magufuli jembe umeliacha shambani namuomba Mungu ampe nguvu
na uwezo mkubwa Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kukamilisha na
kuendeleza kazi iliyobaki shambani tutakukumbuka kwa wema wote
uliotufanyia watanzania na utabaki kuwa shujaa katika taifa letu.
Si
rahisi kuoredhesha mambo yote uliyofanya Magufuli, Uchapakazi wako
umesisimua wananchi na ulimwengu mzima leo unaenda Kaburini taifa likiwa
kwenye majonzi makubwa wananchi wote wa Tanzania, Afrika Mashariki na
Dunia nzima wanakulilia ona maandamano makubwa ya watu toka sehemu
mbalimbali wanaomiminika kuja kukuaga na kukusindikiza katika safari
yako ya mwisho duniani, Mungu aiweke roho yako mahali pema peponi,
upumzike kwa amani, Buriani Rais Magufuli, Buriani Rais wa Wanyonge
pumzika kwa amani“ alisema Mpina
Post A Comment: