Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mhe. Geoffrey I.Mwambe leo ametimiza ahadi yake kwa kukabidhi vifaa vya michezo  kwa timu ya MKUTI MARKET FC. vyenye thamani ya zaidi ya Tshs. 2,000,000/=(Milioni Mbili).


Katika kukabidhi vifaa hivyo Mhe.  Waziri aliwakilishwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (W) Masasi wBi. Zainabu Chinowa ambaye aliongozana na Katibu wa Vijana (W) Ndugu Barnaba Ngunda, Katibu UWT (W) Bi. Mwanahamisi Saidi  na Katibu jumuiya ya Wazazi (W) Ndugu - Issa Tuhaulapa. 


Katika hafla hiyo Katibu wa Chama cha Mapinduzi (W) kwa niaba ya Mhe. Waziri , Aliwapongeza timu ya MKUTI MARKET FC kwa jitihada kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha wanakuwa mabingwa wa mkoa wa Mtwara.  


    "Nawapongeza sana kwa hatua kubwa mliyofikia na nawatakia kila la kheri katika mashindano yenu. Sisi kama Chama cha Mapinduzi, michezo ni moja ya sera yetu Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi  na kwa hakika Mhe. Geoffrey Mwambe anadhihirisha hili kwa kulitekeleza kwa vitendo"


*"Nawasihi viongozi wa MKUTI MARKET FC kuvitunza vifaa hivi ili viweze kuwa chachu ya mafanikio ya timu yenu."*


Baada ya maneno hayo ya faraja na pongezi, kwa niaba ya Mheshimiwa Geoffrey Mwambe (MB), Katibu wa Chama cha Mapinduzi (W) aliwakabidhi vifaa vifuatavyo  :- 

       (a) Jezi Seti 2(Full) 

       (b) Bips 40 

       (c) Shield guard 20 

       (d) Mipira 4 

       (e) Cone za Mazoezi 

       (d) Soksi Set 2 


Katika tukio hili pia Katibu wa Chama (W) kwa niaba ya Mheshimiwa Geoffrey Mwambe (MB), aliongoza HARAMBEE ya kuchangia timu hiyo na kufanikiwa kupata kiasi cha Tshs. 1,550,000/=


Akitoa salamu za shukrani , Mlezi wa timu hiyo Bw. MAHAFUDHI alisema "Tunaishukuru sana Ofisi ya Mbunge Jimbo la Masasi Mjini kwa ushirikiano mzuri wanaotupatia toka mwanzo mpaka sasa , hakika sisi tunawaahidi ushindi mkubwa na kuhakikisha tunasonga mbele.


Pia alitoa rai kwa wadau wengine ndani na nje ya mkoa, kuichangia timu yao kwa kuwa inawakilisha mkoa wa Mtwara.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MKUTI MARKET FC, amemshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Geoffrey Mwambe(MB) kwa juhudi zake za kuendeleza michezo ambayo aliielezea kuwa, siyo burudani tu, bali MICHEZO NI AJIRA.


Aidha, amemsifu kwa kuwa muungwana kwa kuziishi ahadi zake na sasa anazitekeleza moja baada ya nyingine.

 Ameahidi wao kama timu, wataendelea kumuunga mkono katika kuijenga Masasi Mpya.


Hii ni mara ya kwanza kwa Jimbo la Masasi Mjini kutoa mabingwa wa mkoa katika miaka ya karibuni ambapo soka la mkoa wa Mtwara lilionekana kutawaliwa na Tandahimba na Mtwara Manispaa.


Timu hiyo imeanza safari yao jioni ya leo kuelekea Lindi kwa ajili ya kambi na tayari kwa mashindano ambapo mchezo wao wa kwanza utapigwa TAREHE 05/03/2021 katika dimba la ILULU Manispaa ya LINDI.


Tunawatakia kila la kheri MKUTI MARKET FC ambao ni wawakilishi wetu wa mkoa wa Mtwara.


Masasi Mpya...Kazi inaendelea


Imetolewa na:

Ofisi ya Mbunge Jimbo la Masasi Mjini

Share To:

msumbanews

Post A Comment: