UONGOZI wa Mkoa wa Mbeya umepongezwa kwa usimamizi mzuri na hatua kubwa iliyofikiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo jipya la huduma ya wazazi katika hospitali ya wazazi ya Meta. Aidha, hatua iliyofikiwa ni 88% kwa miezi 20 tu kati ya 24 iliyokadiriwa kutumika huku hatua hiyo ikiwa imetumia bilioni 6.4 kati ya bilioni 9 zilizotarajiwa ili kukamilisha mradi huo.
Pongezi hiyo zimetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kutembelea mradi huo ambao unajengwa kwa utaratibu wa ‘force account’.
Dkt. Gwajima alisema ameridhishwa na ujenzi huo kwani ni wa viwango na umaliziaji wake ni mzuri na kasi ya ujenzi wake ni nzuri. Hii inaonesha timu ya mkoa imejipanga vizuri kwenye usimamizi.
“Nimefurahishwa sana na ujenzi huu kwa mkoa wa Mbeya haya ni mapinduzi makubwa katika kuendelea huduma za afya ya uzazi na mtoto, nilikwishakupita hapa miaka ya nyuma hali ilikua tete kwenye jengo la zamani. Mkoa mmefanya kazi kubwa na nzuri, jengo linavutia"
Mkoa mmetengeneza Kamati makini ya kununua vifaa katika kusimamia dhana ya force account, kwakweli nimefurahi.” Aliongeza.
Alisema hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na vyumba 223 kwa ajili ya huduma, vyumba vya upasuaji vitatu, vyumba maalumu (VIP ),wodi ya kujifungua pamoja na wodi ya wagonjwa mahututi (ICU)." Kwahiyo mama mjamzito akiingia humo ndani kila kitu kitaishia humo hata kama atatakiwa kuwa kwenye uangalizi maalumu".
Hata hivyo Dkt. Gwajima alisema yapo mapinduzi na maboresho makubwa ya ujenzi yaliyofanywa na Serikali nchi nzima katika dhana ya kuendeleza afya ya mama na mtoto kwenye halmashauri kuanzia kwenye zahanati mpaka hospitali za wilaya na mkoa ambapo vituo hivyo vina uwezo wa kufanya upasuaji.
“ Hata kwenye jamii kuna wahudumu wa afya ya jamii wanaofuatilia masuala ya afya ya watoto na wazazi na kutoa ushauri. Serikali kwa kushirikiana na wananchi imejenga zahanati 1198 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015, vituo vya afya 487 vyenye uwezo wa kufanya upasuaji na vituo vingi vimeanza kutoa huduma hiyo na vile ambavyo bado tunaenda kuviwezesha vianze kutoa huduma hiyo mara moja kwani Serikali imedhamiria kumuokoa mtoto na mwanamke ili waachane na changamoto za kupoteza maisha ya watoto wakiwa tumboni au mwanamke anapojifungua ”. alisisistiza
Naye Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila alisema kukamilika kwa jengo hili litasaidia sana kufuta vifo vya mama na mtoto Kwenye mkoa wake kwani jengo hilo litakua na vifaa na vifaa tiba na kuongeza kuwa hadi sasa malalamiko ya akina mama kuhusiana na uzazi yamepungua licha ya ufinyu wa jengo lililopo.
Mhe. Chalamila alisema takwimu zinaonyesha akina mama wanaofika kujifungua kwenye hospitali hiyo kwa mwezi ni akina mama zaidi ya mia sita na hospitali hiyo imeweza kushusha vifo vitokana vyo na uzazi hivyo anaishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao unaenda kuwaokoa akina mama na Watoto wa Mkoa wake.
Katika ziara yake mkoani hapa Dkt. Gwajima alitembelea pia hospitali ya rufaa ya mkoa Mbeya na kujionea hali ya ujenzi wa jengo la upasuaji lenye vyumba sita vya upasuaji na jengo la dharura na ameahidi wizara itafanya mpango wa ujenzi wa jengo la uzazi kwenye hospitali hiyo ya mkoa ili kuweza kuwapunguzia mzigo hospitali ya wazazi ya meta ambayo ipo chini ya hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya.
Post A Comment: