Maofisa wawili wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Kilimanjaro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakikabiliwa na makosa mbalimbali yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh. Milioni 18.
Maofisa hao waliokuwa Idara ya Uhasibu katika Gereza Kuu la Karanga wamefikishwa mahakamani jana Jumatatu Machi 29, 2021 na kusomewa mashtaka yao na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Samwel Gabriel mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Jenifer Edward.
Watuhumiwa hao walofikishwa mahakamani ni mrakibu msaidizi (ASP) Ibrahim Ukoko (43) na Inspekta msaidizi, Jacob Shirima (44).
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha mashtaka Gabriel amedai kuwa mshtakiwa wa kwanza ASP Ukoko anadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 18 na 21 mwaka 2018, alighushi barua mbili zenye kichwa cha habari ‘kutoa pesa kwenye akaunti kwa matumizi ya ofisi’.
Amedai kuwa mshtaiwa huyo wa kwanza akiwa Idara ya Uhasibu alitaka kuonyesha kuwa barua hiyo ilikuwa imeandikwa na mkuu wa gereza (RPO) maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo.
Gabriel amedai, Desemba 24, 2018 mshtakiwa huyo anadaiwa kutumia hati ya malipo yenye namba 207/12 iliyokuwa na maelezo ya uongo kwamba Sh18, 650,900 zinapaswa ziingizwe kwenye akaunti ya RPO Kilimanjaro.
Mwendesha mashtaka huyo amedai maelezo hayo yalikuwa ni ya uongo yenye lengo la kumdanganya mwajiri wake ambaye ni Serikali.
Ilidaiwa pia washtakiwa wote wawili walishirikiana kufanikiwa kutoa benki fedha kwa awamu mbili za Sh11 milioni na Sh7 milioni, fedha mbazo walizitumia kwa manufaa yao wenyewe na kuisababishia mamlaka hasara ya Sh18 milioni.
Hata hivyo mara baada ya kusomewa mashtaka yao watuhumiwa hao walikana kutenda makosa hayo.
Hakimu Edward aliwaeleza mahakama hiyo haina uwezo kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, kuwataka waende mahakama kuu kuomba dhamana na kuamuru wapelekwe katika gereza la Karanga hadi Aprili 4, 2021.
Taarifa iliyotolewa jana na mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikes inaeleza kuwa washtakiwa walisomewa mashtaka yanayohusiana na kughushi nyaraka, ufujaji na ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri.
Post A Comment: