Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) inaendesha mafunzo ya kitaifa juu ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia mahala pa kazi kwa wafanyakazi 45 wanaotumia vyanzo vya mionzi katika sekta za Viwanda, Utafiti na Migodi.
Mafunzo hayo yaliyoanza leo jumatatu tarehe 15 Machi 2021 Makao Makuu ya TAEC, Jijini Arusha yatafikia kilele siku ya ijumaa tarehe 19 Machi 2021.
Malengo ya mafunzo hayo ni kutoa ufahamu juu ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi, kuwapa maarifa mapana juu ya utumiaji salama wa teknolojia ya Nyuklia, kutambua athari za kibaolojia za mionzi, kutambua kanuni za kitaifa na kimataifa za udhibiti wa mionzi na vilevile kutambua matumizi salama na usafirishaji wa vyanzo vya mionzi.
Akifungua mafunzo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkuu wa Mafunzo na Utafiti, Dkt. Shovi Sawe amesema mafunzo hayo yatawajengea washiriki ufahamu wa matumizi salama wa vyanzo vya mionzi ili kuchukua tahadhali na kuendelea kujilinda dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi kwenye maeneo yao ya kazi.
“Nina imani mafunzo haya yatawasaidia katika kupata ujuzi kwani mtapata uzoefu mkubwa kutoka kwa wataalamu wa TAEC ambao watawafundisha masuala mbali mbali ya ulinzi na usalama kwenye vyanzo vya mionzi mnavyotumia,” alisema Dk. Sawe.
Kwa upande wake, mratibu wa mafunzo hayo, Bwana Atumaini Makoba amesema washiriki hao mbali na kufundishwa kwa nadharia pia watapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo jambo ambalo litawasaidia ili kuwaongezea ulewa kwenye mafunzo hayo.
Post A Comment: